Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Bw. George Nyatega (mwenye tai) akipokea tuzo kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU) - Tawi la HESLB Bw. Deodatus Mwiliko kutambua uongozi wake bora katika HESLB tangu ilipoanzishwa mwaka 2005. Wengine ni viongozi wa RAAWU-HESLB Bw. Luhano Lupogo na Bi. Octavia Selemani.
Na Mwandishi wetu
Watumishi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wametakiwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuondokana na malalamiko kutoka kwa wanafunzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. George Nyatega ametoa wito huo mara baada ya kukabidhiwa tuzo na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU), tawi la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).
Akiongea katika hafla fupi ya kukabidhi ngao hiyo, Mwenyekiti wa RAAWU Tawi la HESLB Bw. Deodatus Mwiliko alisema RAAWU, Tawi la HESLB imeamua kumkabidhi Mkurugenzi mtendaji huyo ngao hiyo kutokana na kujali na kuboresha mazingira ya kufanya kazi kwa watumishi wote wa HESLB.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji huyo alisema amepokea tuzo hiyo kwa niaba ya menejimenti anayoingoza na wafanyakazi wote na kuwataka watumishi wa HESLB kutoridhika na ufanisi uliopo na badala yake waongeze juhudi.
“Ninapokea hii ngao kwa niaba ya menejimenti na wafanyakazi wote kwa sababu sifanyi kazi peke yangu,” alisema Bw. Nyatega leo (Alhamisi, Mei 28, 2015) katika makao makuu ya HESLB jijini Dar es Salaam.
“Ninawapongeza kwa kufanya kazi kwa ufanisi, lakini pia muongeze juhudi katika utoaji wa huduma kwa wanafunzi ili pasiwe na malalamiko,” amesema Bw. Nyatega.
HESLB ilianzishwa kwa sheria ya Bunge na 9 ya mwaka 2004 na kuanza kazi rasmi mwezi Julai, 2005 ili, pamoja na majukumu mengine kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji waliodahiliwa katika taasisi za elimu ya juu. Tangu kuanzishwa kwake, Bw. Nyatega amekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake.
0 comments:
Post a Comment