WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amepokea msaada wa vitabu 895 vyenye thamani ya sh. milioni 6.5/- ikiwa ni jitihada ya wadau mbalimbali kuchangia shule ya msingi aliyosoma ya Kakuni iliyoko kijiji cha Kibaoni, wilayani Mlele, mkoani Katavi.
Waziri Mkuu amepokea msaada huo jana mchana (Jumanne,
Mei 26, 2015) kwenye shule mpya ya msingi Kakuni ambayo bado inaendelea
kujengwa kwenye kijiji cha Kibaoni.
Akizungumza
katika hafla hiyo fupi mara baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu Pinda
aliishukuru kampuni ya General Booksellers Ltd ya kutoka Dar es Salaam kwa
msaada huo ambao alisema utachangia kwa kiasi kikubwa kuitimiza ndoto yake
aliyokuwa nayo ya kuisaidia jamii iliyomsomesha.
“Wazo
la ujenzi wa shule mpya ya msingi Kibaoni lilitokana na ukweli kwamba nilisoma
na kumaliza kwenye shule hii ya Kakuni. Nikiwa ni mtumishi wa Serikali, ni
Mbunge na sasa hivi ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
nilijiuliza hivi shule hii ninaweza kuiacha hivi hivi?”
“Nilijiuliza
sana ni jambo gani ambalo naweza kulifanya la kusaidia wanakijiji wenzangu na
kata nzima ya Kibaoni kama shukrani kwa kunilea na kunifikisha hapa nilipo.
Ndipo wazo la kujenga shule niliyosoma likazaliwa kama mwaka mmoja na nusu
uliopita,” alisema Waziri Mkuu wakati akiwahutubia wazazi, walimu na wanafunzi.
0 comments:
Post a Comment