Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
imeanza kukagua taasisi za umma kuhusu utekelezaji wa sheria inayozitaka
kuwatambua waajiriwa walionufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Hadi
Mei mwaka jana, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)
ilikuwa imekusanya Sh65.2 bilioni kati ya Sh123.8 bilioni zilizopaswa
kuwa zimerejeshwa.
Bodi hiyo iliwakopesha wanafunzi
Sh1.8 trilioni tangu mwaka wa masomo 1994/95 hadi Juni 2014 kati ya
fedha hizo, Sh51 bilioni zilitolewa na iliyokuwa Wizara ya Elimu ya Juu,
Sayansi na Teknolojia.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB,
George Nyatega alisema ili kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mikopo
iliyoiva, CAG ameanza kutekeleza matakwa ya kisheria ya ukaguzi kwenye
taasisi za umma ili kuwabaini wanafunzi waliopaswa kuanza kurejesha
mikopo yao.
“Ni imani ya HESLB kuwa waajiri katika
utumishi wa umma watatoa ushirikiano kwa ofisi ya CAG ili kuondokana na
matatizo ya kisheria,” alisema.
Nyatenga alisema sheria
iliyoanzisha HESLB inazitaka taasisi zote za umma kuijulisha kwa
maandishi kuhusu waajiriwa wapya ndani ya siku 28 na bodi kuthibitisha
kama waajiriwa hao ni wanufaika wa mikopo au la.
Mkurugenzi
huyo alisema baada ya bodi kupokea taarifa na kuthibitisha kuwa
waajiriwa ni wanufaika wa mikopo, mwajiri atapaswa kuijulisha HELSB na
kuanza kukata sehemu ya mshahara wa mwajiriwa ndani ya siku 30.
0 comments:
Post a Comment