Shule ya Wasichana Songwe Yang’ara kwa Ufaulu wa Asilimia 100

Wadau mbalimbali wa elimu wakiwa katika mikutano na Wanafunzi wa baadhi ya Shule za wilayani Momba, ambapo maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yanafanyika.

Na Mwandishi Wetu, Songwe

Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yanaendelea mkoani Songwe huku wadau mbalimbali wa elimu wakitembelea shule na kujionea maendeleo pamoja na changamoto zinazokabili sekta hiyo.

Katika ziara hiyo, Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) pamoja na wadau wengine wa elimu walitembelea Shule ya Wasichana Songwe iliyopo wilayani Momba, shule ambayo imeendelea kung’ara kitaaluma tangu kuanzishwa kwake.

Akizungumza mbele ya wageni hao, Mkuu wa Shule hiyo, Bi. Janeth Mwamwile, alisema shule hiyo ilianza ikiwa na wanafunzi 25 chini ya usimamizi wa mkoa, lakini sasa imekua hadi kufikia wanafunzi 161 pamoja na walimu 15 wenye dhamira ya kuinua elimu ya mtoto wa kike.

Alisema kwa miaka minne mfululizo shule hiyo imekuwa ikipata ufaulu wa asilimia 100, jambo lililoifanya kujizolea sifa katika ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, Bi. Mwamwile alisema shule bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali za miundombinu ikiwemo ukosefu wa nyumba za walimu, maabara, bwalo la chakula, mabweni, jengo la utawala pamoja na jiko.

Aliwataka wadau wa elimu na jamii kwa ujumla kuunga mkono jitihada za shule hiyo ili kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET), Bi. Martha Makala, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike ili kuwajengea msingi imara wa maisha ya baadaye.

Alisema yeye mwenyewe ni mfano wa mafanikio yaliyotokana na kusoma katika shule ya wasichana, hivyo ni muhimu kuendelea kuwawezesha wasichana kutimiza ndoto zao.

Bi. Makala pia aliahidi kuwa changamoto zilizowasilishwa na shule hiyo zimepokelewa rasmi na zitafanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ili kutafuta suluhisho la kudumu.

Maadhimisho ya Juma la Elimu Kitaifa yamekuwa jukwaa muhimu la kujadili mafanikio, changamoto na mikakati ya kuimarisha sekta ya elimu nchini.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment