Black Swan Yawasaidia Wasio kwenye Mfumo Rasmi wa Benki Kupata Mikopo

Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM — Kampuni ya teknolojia ya kifedha ya Black Swan-Tanzania imeingia kwenye orodha ya kampuni 25 bora zinazochipukia barani Afrika kwa mwaka 2026 iliyotolewa na taasisi kubwa ya habari za fedha duniani, Bloomberg.

Black Swan, kampuni iliyosajiliwa Tanzania na inayojihusisha na huduma za kifedha kupitia teknolojia ya akili mnemba (AI), imetambuliwa kutokana na mchango wake wa kurahisisha upatikanaji wa mikopo nafuu na ya haki kwa Waafrika ambao bado hawajahudumiwa kikamilifu na mifumo rasmi ya kifedha.

Orodha hiyo ya Bloomberg hutambua kampuni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika zinazotatua changamoto muhimu kwa kutumia teknolojia na ubunifu wenye matokeo chanya katika jamii na uchumi.

Kupitia teknolojia yake, Black Swan hubadilisha taarifa za miamala ya kifedha inayofanyika kwenye simu za mkononi kuwa taarifa zinazoweza kusaidia taasisi za fedha kufanya tathmini sahihi za mikopo kwa wananchi na wafanyabiashara wadogo ambao mara nyingi hawapo kwenye mfumo rasmi wa benki.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mwanzilishi Mwenza na Afisa Mkuu Mtendaji wa Black Swan, Derick Kazimoto, alisema kutambuliwa huko ni ishara kuwa dunia inaanza kuona mchango wa kampuni hiyo katika kuboresha ujumuishaji wa kifedha barani Afrika.

“Tunafurahia kuona juhudi zetu zinatambulika kimataifa. Mamilioni ya Watanzania wanafanya kazi na biashara kila siku lakini bado hawaonekani katika mifumo rasmi ya fedha. Tuliianzisha Black Swan kubadilisha hali hiyo,” alisema Kazimoto.

Alisema teknolojia ya kampuni hiyo inachakata taarifa za kifedha kwa usalama na kwa idhini ya watumiaji ili kusaidia wakopeshaji kufanya maamuzi ya haraka, sahihi na yenye uwazi zaidi.

Kwa sasa Black Swan inahudumia zaidi ya taasisi 30 za kifedha Afrika Mashariki katika tathmini za mikopo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo mikopo midogo, mikopo ya kidijitali, ufadhili wa magari na mali nyingine pamoja na huduma za kawaida za mikopo.

Miongoni mwa bidhaa zake kuu ni “Kopa Gari”, mfumo wa kidijitali unaorahisisha upatikanaji wa mikopo ya magari ambapo majibu ya awali ya ustahiki wa mkopo hutolewa ndani ya dakika tano pekee.

Kampuni hiyo pia imeanzisha mfumo wa “Manka”, unaotumia akili mnemba kusaidia wakopeshaji kupata taarifa sahihi kuhusu uwezo wa mkopaji kulipa, hali inayosaidia kuongeza kasi na usahihi wa utoaji wa mikopo.

Kutambuliwa kwa Black Swan kunakuja wakati kampuni changa za teknolojia Afrika zikiendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya bara hilo kutokana na mchango wao katika maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

Kupitia mafanikio hayo, Tanzania imeendelea kujijengea nafasi kwenye ramani ya ubunifu wa teknolojia Afrika sambamba na mataifa kama Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Morocco yaliyowakilishwa katika orodha hiyo ya Bloomberg.

SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment