Ridhiwani Kikwete Atoa Wito kwa Wahitimu Kuwa Viongozi Waadilifu

Na Jawadu Kinyobwa 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete amewataka wahitimu wa Taasisi ya Uongozi kuwa viongozi waadilifu, wenye nidhamu na uthubutu ili kuchangia maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Akizungumza Mei 15, 2026 katika Mahafali ya Tisa ya Taasisi hiyo yaliyofanyika katika Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mhe. Ridhiwani alisema dunia ya sasa inahitaji viongozi wenye maadili, uwajibikaji na uwezo wa kufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.

Alisema uadilifu ni sifa muhimu ya kiongozi bora na mwenye kuaminika, hivyo wahitimu wanapaswa kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwa viongozi wanaozingatia haki, uwazi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.“Nawakumbusha umuhimu wa kuwa viongozi wenye uzalendo. Tukumbuke msemo wa wahenga kwamba adhabu ya msaliti ni malipo ya usaliti wake. Usaliti mkubwa katika uongozi wa umma ni sawa na ubadhirifu wa mali za umma,” alisema Ridhiwani. 

Aidha, aliwataka wahitimu hao kulinda rasilimali za taifa na kuweka mbele maslahi ya wananchi katika maamuzi yao ya kila siku ili kusaidia kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Alisema Tanzania inahitaji viongozi waaminifu na wenye uwajibikaji ambao watatumia nafasi zao kuendeleza ustawi wa wananchi na kuimarisha misingi ya utawala bora.
Sambamba na hilo, Waziri Ridhiwani alisema uongozi unaozingatia haki na uwazi utaendelea kuitangaza vyema Tanzania pamoja na Taasisi ya Uongozi ndani na nje ya nchi.

Awali akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Bw. Kadari Singo alisema taasisi hiyo imetimiza miaka 15 tangu kuanzishwa kwake rasmi Julai mwaka 2010 kwa Hati ya Rais kama Kituo cha Utaalamu wa Hali ya Juu kwa ajili ya kujenga na kuimarisha viongozi barani Afrika.

Alisema kwa kipindi hicho, taasisi hiyo imefanikiwa kutoa mafunzo mbalimbali ya uongozi, kuandaa mijadala ya kisera pamoja na kufanya tafiti na machapisho yaliyosaidia kukuza maarifa ya kiuongozi.

Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya wahitimu, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), Juma Burhan Mohamed alisema mafunzo hayo yamewajengea uwezo mkubwa wa kiuongozi na kuwasaidia kufanya maamuzi yenye tija kwa taasisi na jamii.

Alisema mahafali hayo hayakuwa tu hitimisho la mafunzo, bali yalikuwa ishara ya mabadiliko makubwa ya kiuongozi na maendeleo binafsi waliyoyapata ndani ya miezi sita ya programu hiyo.











SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment