TRAMEPRO: Kuwathamini akina mama ni msingi wa maendeleo endelevu

 

Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limesema linaendelea kutambua na kuthamini nafasi kubwa ya wanawake na akina mama katika uhifadhi wa mimea dawa, malezi ya maadili ya jamii pamoja na ustawi wa familia na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo, wakati akitoa salamu za maadhimisho ya Siku ya Mama Duniani ambayo huadhimishwa kila Jumapili ya pili ya mwezi Mei.

Mwalongo amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kutambua mchango mkubwa wa mama katika maisha ya mwanadamu na maendeleo ya jamii, huku akieleza kuwa historia inaonyesha siku hiyo ilianzishwa kupitia juhudi za Anna Jarvis nchini Marekani mwanzoni mwa karne ya 20.

Amesema katika maadhimisho ya mwaka 2026, TRAMEPRO inawakumbusha wananchi kuendelea kuwaheshimu, kuwathamini na kuwaenzi akina mama kutokana na mchango wao mkubwa katika afya, elimu, kilimo, mazingira, malezi na maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.

“TRAMEPRO inaamini kuwa jamii yenye kuwathamini wanawake na akina mama ndiyo msingi wa Taifa lenye maadili, afya njema na maendeleo endelevu,” amesema Mwalongo.

Aidha, amesema kauli ya kutafakari mwaka 2026 ni: “Upendo wa Mama ni msingi wa familia imara na jamii yenye utu.”

Katika salamu zake, Mwalongo pia alitoa dua maalumu kwa akina mama wote duniani huku akimuombea aliyekuwa mama yake mzazi, marehemu Ostela Sanga, apumzike mahali pema peponi.

SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment