
Na Mwandishi Wetu, Siha
Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro
inatarajiwa kupokea zaidi ya washiriki 800 kutoka ndani na nje ya
Tanzania katika mashindano makubwa ya michezo na utalii yajulikanayo
kama West Kili Forest Tour Challenge, yatakayofanyika Juni 20 hadi 21,
2026 katika ukanda wa msitu wa West Kilimanjaro.
Mashindano hayo
yamezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Siha, Dkt. Christopher Timbuka,
aliyesema tukio hilo litakuwa chachu ya kuitangaza Siha kimataifa
kupitia utalii wa asili, michezo na shughuli za kijamii zitakazochochea
uchumi wa wananchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt.
Timbuka alisema mashindano hayo yatahusisha mbio za kilomita 5, 10 na
21, pamoja na mashindano ya baiskeli na pikipiki yatakayopita katika
maeneo yenye mandhari ya kuvutia ya msitu wa West Kilimanjaro.
“Tunatarajia
kupokea washiriki wengi kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania na nje ya
nchi. Hii ni fursa kubwa kwa Siha kuendelea kujitangaza kama kitovu cha
utalii wa michezo na uhifadhi wa mazingira,” alisema Dkt. Timbuka.
Aliongeza
kuwa maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha mashindano
hayo yanafanyika kwa mafanikio makubwa huku yakitoa nafasi kwa wananchi
kunufaika kupitia biashara mbalimbali zikiwemo malazi, chakula, usafiri
na huduma nyingine za kijamii.
Kwa mujibu wa waandalizi, kabla ya
siku ya mashindano kutafanyika mkesha maalumu wa burudani
utakaojumuisha shughuli za kijamii, muziki, chakula na vinywaji kwa
washiriki na wadau mbalimbali.
Mashindano hayo yanaungwa mkono na
kampuni ya Mati Super Brands Ltd ambayo imeahidi kushirikiana
kuhakikisha tukio hilo linakuwa la kipekee na lenye mafanikio makubwa.
Akizungumza
kuhusu malengo ya mashindano hayo, Mratibu wa West Kili Forest Tour
Challenge, Bw. Mensier Elly, alisema tukio hilo si la michezo pekee bali
ni jukwaa muhimu la kutangaza vivutio vya utalii vya West Kilimanjaro
na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kupitia michezo na utalii endelevu.
“Tunataka
kutumia michezo kama njia ya kuhamasisha jamii kuthamini mazingira na
wakati huo huo kuitangaza West Kilimanjaro kwa dunia,” alisema Bw. Elly.
Mashindano
hayo yanatarajiwa kuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo na
utalii nchini mwaka huu kutokana na ushiriki mkubwa unaotarajiwa pamoja
na mvuto wa kipekee wa mazingira ya West Kilimanjaro.


Mbunge wa Jimbo la Siha mkoani Kilimanjaro, Dkt. Godwin Mollel akitoa neno.
Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti West Kilimanjaro, PCO Robert Faida akisoma risala.
Mratibu wa West Kili Forest Tour
Challenge, Bw. Mensier Elly
















0 comments:
Post a Comment