Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akisalimiana na Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho wa kibalozi katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Katikati ni Mheshimiwa Ahmed Attaf, Waziri wa Mambo wa Nje wa Algeria.
Mheshimiwa Balozi Mobhare Matinyi akizungumza na waandishi wa habari wa Algeria mara baada ya kukabidhi hati zake za utambulisho wa kibalozi kwa Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algiers tarehe 10 Juni, 2026. Kushoto kwake ni Mwambata wa Ulinzi Kanali Nassoro Kapolo na kushoto kwake ni Afisa wa Ubalozi, Maryam Kilongo.
Na Mwandishi Wetu
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amekabidhi hati zake za utambulisho wa kibalozi kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Abdelmadjid Tebboune, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Algiers, Juni 10, 2026, kuashiria kuanza rasmi kwa majukumu yake ya kuiwakilisha Tanzania nchini humo.
Baada ya hafla hiyo, Balozi Matinyi alimfikishia Rais Tebboune salamu na shukrani kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuthamini uhusiano wa kindugu na ushirikiano uliodumu kwa zaidi ya miaka 60 kati ya Tanzania na Algeria.
Akizungumza na waandishi wa habari, Balozi Matinyi alisema mazungumzo yao yalijikita katika namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano uliopo, hasa baada ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta za ulinzi na elimu ya juu. Alisema pande hizo mbili zimekubaliana kuweka msukumo mpya katika sekta nyingine zenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi.
Alitaja maeneo ya kipaumbele yaliyopatiwa msisitizo kuwa ni kilimo, viwanda, utengenezaji wa dawa, nishati, madini na utalii, pamoja na kuendeleza ushirikiano katika sekta za sayansi, teknolojia, utafiti, utamaduni na elimu ili kuimarisha mahusiano baina ya mataifa hayo mawili.
"Nimepewa jukumu na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha ushirikiano wa Tanzania na Algeria unawanufaisha wananchi wa pande zote mbili. Kwa kutumia umahiri wa viongozi wetu, tunaamini tutafanikisha azma hiyo," alisema Balozi Matinyi.
Kwa upande wake, Rais Tebboune alieleza utayari wa Algeria kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika sekta mbalimbali za maendeleo, akibainisha kuwa nchi yake iko tayari kufikia makubaliano mapya kupitia vikao vya pamoja na ziara za viongozi wa ngazi za juu.
Balozi Matinyi anakuwa balozi wa nne wa Tanzania nchini Algeria, akitanguliwa na Balozi Omari Yussuf Mzee, Meja Jenerali Jacob Kingu na Balozi Imani Njalikai. Mbali na Algeria, Ubalozi wa Tanzania uliopo Algiers unahudumia pia nchi za Tunisia, Mauritania, Niger na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (SADR).


0 comments:
Post a Comment