EY Tanzania imezindua kwa mafanikio Ripoti ya Sekta Ndogo ya Benki Tanzania 2025, tukio lililowakutanisha viongozi wa sekta ya fedha, wadhibiti na wataalamu wa benki kujadili mwelekeo wa sekta hiyo katika mazingira yanayobadilika kwa kasi. Mada kuu ya mwaka huu ilikuwa“Akili Mnemba katika Sekta ya Benki: Faida ya Ushindani Ijayo”, ikilenga kuonesha jinsi Akili Mnemba (AI) inavyobadilisha ushindani katika huduma za kifedha.
Majadiliano hayo yaliongozwa na Bi. Irene Morris (EY) ambapo aligusia safari ya mageuzi ya sekta ya benki kutoka mifumo ya jadi inayotegemea mahusiano ya karibu na wateja (relationship banking) hadi benki za kidijitali, majukwaa ya kifedha (platform banking) na mifumo ya ikolojia ya huduma za kifedha (ecosystem banking). Washiriki walijadili namna AI, data na teknolojia vinavyoboresha uzoefu wa wateja, kuimarisha usimamizi wa hatari, kuongeza ufanisi wa shughuli za benki na kuibua fursa mpya za ukuaji wa biashara.

Tukio hilo pia liliangazia mwenendo muhimu unaoendelea kuunda sekta ya benki nchini Tanzania, ikiwemo ukuaji endelevu wa sekta, kuongezeka kwa ujumuishaji wa kifedha, matumizi yanayoongezeka ya huduma za kifedha za kidijitali, pamoja na umuhimu wa ubunifu katika kujenga taasisi za kifedha zilizo imara na zenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya siku zijazo.
Aidha, washiriki walipata fursa ya kujadili kiwango kipya cha utoaji taarifa za kifedha (IFRS 18) na athari zake kwa sekta ya benki. Majadiliano yalioongozwa na Bw. Joshua Luoga (EY) ambapo alitoa ufahamu kuhusu mabadiliko yajayo katika uwasilishaji wa taarifa za kifedha, upimaji wa utendaji wa kifedha pamoja na kuongeza uwazi kwa wadau wa sekta ya fedha.
EY Tanzania inawashukuru kwa dhati wazungumzaji, (Bw. Rweyemamu Barongo, Kiongozi wa Kitengo cha Ubunifu wa Akili Mnemba (AI) na Data katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dkt. Tobias Swai, Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Fedha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Pamoja na Bw. Robert Bwana, Mwanasayansi Mwandamizi wa Data katika Benki ya NMB) washiriki na wadau wote waliochangia mjadala wenye tija kuhusu mustakabali wa sekta ya benki nchini Tanzania na nafasi ya teknolojia na ubunifu katika kuendeleza ukuaji wa sekta hiyo.














0 comments:
Post a Comment