Vodacom Tanzania yazindua kampeni ya "Zaidi ya Mtandao", Ikiimarisha dhamira yake ya kuleta fursa zaidi ya huduma za mawasiliano

 

Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa Vodacom Tanzania Plc Brigita Shirima (katikati), Mkurugenzi wa Vodacom Business wa kampuni hiyo Nguvu Kamando (kulia), pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa Tulisindo Mlupilo (kushoto) wakiwa kwenye picha ya pamoja wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya "Zaidi ya Mtandao" yenye lengo la kuimarisha dhamira ya kuleta fursa na huduma kwa wateja wake ikiwa ni zaidi ya huduma za mawasiliano ila ni suluhisho halisi la maisha ya kila siku kwa jamii. Tukio hilo limefanyika leo tarehe 4 August 2026, Makao makuu ya Vodacom Tanzania Plc, jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, Tanzania, Agosti 4, 2026: Vodacom Tanzania Plc leo imezindua rasmi kampeni yake ya "Zaidi ya Mtandao" (More Than a Network), hatua inayodhihirisha dhamira ya muda mrefu ya kampuni ya kutoa zaidi ya huduma za mawasiliano kwa kuwezesha fursa kwa watu, biashara na jamii mbalimbali nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa robo ya mwaka iliyoishia Machi 2026, Vodacom iliendelea kuongoza soko la mawasiliano nchini kwa kuwa na asilimia 32.3 ya wateja wote, sawa na zaidi ya wateja milioni 36.1. Aidha, kwa mujibu wa taarifa ya fedha ya kampuni kwa robo ya mwaka iliyoishia Juni 2026, Vodacom imeongeza uwekezaji wake karibu mara mbili ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita, ambapo uwekezaji ulifikia shilingi bilioni 123.2. Uwekezaji huo, sambamba na maboresho makubwa ya mfumo wa M-Pesa, unaonesha dhamira ya kampuni ya kutekeleza falsafa ya "Zaidi ya Mtandao" kwa kuharakisha ujumuishaji wa kidijitali nchini na kuwezesha Watanzania wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Kitengo biashara wa Vodacom Tanzania Plc, Brigita Shirima, alisema kampeni hiyo inaakisi dhamira ya Vodacom ya kuhakikisha teknolojia inaleta thamani halisi na matokeo chanya kwa wateja.

“Zaidi ya Mtandao” ni ahadi yetu kwamba teknolojia na huduma tunazotoa lazima zilete matokeo chanya. Iwe ni kumsaidia mwanafunzi kupata elimu ya kidijitali, kuwezesha familia kuendelea kuwa karibu au kusaidia wajasiriamali kukuza biashara zao, tunalenga kuunda fursa zinazoboresha maisha. Kwa sababu mtandao haupimwi kwa teknolojia pekee, bali kwa thamani na fursa unazozalisha kwa watu, biashara na jamii," alisema Shirima

Akizungumzia mchango wa suluhisho za kidijitali katika kukuza biashara, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, alisema mabadiliko ya kidijitali si jambo linalohusu mashirika makubwa pekee, bali yanazalisha na kufungua fursa katika sekta mbalimbali za uchumi ndani ya jamii.

“Biashara za leo zinahitaji zaidi ya huduma wa mawasiliano. Zinahitaji suluhisho za kidijitali zinazowasaidia kubuni, kushindana na kukua. Kupitia Vodacom Business, tunawezesha kampuni, biashara ndogo na za kati pamoja na taasisi mbalimbali kwa huduma salama za mawasiliano, teknolojia ya utunzaji wa kumbukumbu, teknolojia ya vifaa vilivyounganishwa (Internet of Things - IoT) na majukwaa ya kidijitali yanayoongeza ufanisi na kufungua fursa za kiuchumi. Kwetu, ‘Zaidi ya Mtandao’ kunamaanisha kuwa mshirika wa kuaminika wa kidijitali katika safari ya Tanzania kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.” alisema Kamando.

 Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania Plc, Tulisindo Mlupilo, alisema M-Pesa inaendelea kuwa nguzo muhimu ya ujumuishaji wa kifedha kwa kuwawezesha mamilioni ya Watanzania kupata huduma za kifedha kwa urahisi na usalama.

"Mfumo wa M-Pesa unahudumia zaidi ya watumiaji hai milioni 14.1 kila mwezi kupitia huduma zinazowawezesha kuweka akiba kupitia M-KOBA, kupata mikopo kupitia SONGESHA, kuwekeza kupitia M-WEKEZA, kufanya malipo ya biashara kupitia LIPA na kutuma na kupokea fedha kwa urahisi. Maboresho ya mfumo wa M-Pesa yataongeza uwezo wetu wa kutoa huduma za kifedha kwa ufanisi zaidi na kuendelea kuunga mkono juhudi za Tanzania za kujenga uchumi wa kidijitali. Dhamira ya Vodacom ni kuendelea kutumia teknolojia kama chachu ya ujumuishaji wa kifedha na kuongeza thamani kwa wateja wetu, tukiendelea kutekeleza falsafa ya ‘Zaidi ya Mtandao’." alisema Mlupilo.

Vodacom inaamini kuwa thamani ya mtandao haipimwi kwa wigo wa huduma, kasi au teknolojia pekee, bali kwa fursa na matokeo chanya unayowezesha katika maisha ya watu kila siku.

Kadri Vodacom inavyoendelea kuwekeza katika mtandao wake, kuboresha uzoefu wa wateja na kuendeleza suluhisho bunifu za kidijitali, "Zaidi ya Mtandao" itaendelea kuwa msingi wa dhamira ya kampuni ya kuunda fursa, kuwezesha maendeleo na kuboresha maisha ya Watanzania.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment