Makonda Hatambui Jezi Mpya za Taifa Stars, Kamati Kuchunguza Mikataba

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, ametangaza kutoutambua mchakato wa kubadilisha jezi za timu za taifa, akisema umefanyika bila kuishirikisha Wizara licha ya maelekezo aliyoyatoa Februari 2026.

Sambamba na hatua hiyo, Waziri Makonda ameagiza kuundwa kwa kamati maalumu itakayochunguza mikataba ya wazabuni wa jezi hizo, manufaa yake kwa timu za taifa pamoja na mapato yanayotokana na mauzo yake.

Uamuzi huo umetangazwa siku mbili baada ya Waziri Makonda kukataa hadharani jezi mpya zilizoonekana zikivaliwa na Naibu Waziri wa Wizara hiyo, akisema hazikuwa na ubora unaoendana na hadhi ya Taifa Stars.

“Hii siyo jezi ya Taifa Stars. Taifa Stars kwa ubora wake hatuwezi kuwa na jezi za kiwango cha chini hivi. Acheni kutumia picha za Naibu wangu huku ofisi yangu haina taarifa. Tuheshimiane,” alisema Waziri Makonda kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara leo, Septemba 18, 2026, uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo mikataba iliyopo inanufaisha timu za taifa kwa kiwango kinacholingana na fedha nyingi zinazotolewa na Serikali kugharamia timu hizo.

Wizara imeeleza kuwa Februari 2026, Waziri Makonda alitoa maelekezo ya kuboresha jezi za timu za taifa ili ziakisi utambulisho wa Tanzania na kuzalisha manufaa mapana kwa nchi.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa muhimu kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika maandalizi ya timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, pamoja na Tanzania kuwa mwenyeji mwenza wa Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2027 (AFCON 2027).

Kamati hiyo pia itachunguza mapato yanayotokana na mauzo ya jezi na mchango wake katika kugharamia uendeshaji wa timu za taifa.

SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment