Mradi wa maji sh bilioni 53.12 kukamilika novemba 30

Na Oscar Assenga, Tanga

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji wa hati fungani wenye thamani ya Sh bilioni 53.12 kuongeza nguvu kazi na kuhakikisha mradi huo unakamilika ifikapo Novemba 30, 2026, akisisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa nyongeza.

Aweso ametoa agizo hilo wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo, ikiwamo tanki kubwa la maji lililopo Mowe jijini Tanga, ambapo amesema serikali haitakubali visingizio kwa kuwa fedha za utekelezaji wa mradi huo zipo.

Amesema mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 70 ya utekelezaji na kwamba mkandarasi anatakiwa kuongeza kasi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha wananchi wanaanza kunufaika na huduma hiyo kwa wakati uliopangwa.

“Nimekuja leo kukagua huu mradi nikiwa na Katibu Mkuu. Mradi huu sasa umefikia asilimia 75. Maelekezo ambayo nawaambia Tanga Uwasa na mkandarasi ni kwamba hatutakuwa na muda wa nyongeza,” amesema Aweso.
Ameongeza kuwa utendaji wa mradi huo unatakiwa kubadilika na mkandarasi kuongeza wafanyakazi ili kukamilisha kazi kwa wakati, akisisitiza kuwa hakuna sababu ya kuchelewesha mradi kwa kuwa fedha zipo.

“Tunataka mwisho wa mwezi huu wa 10 tukija kuona maendeleo yake, yatupatie picha kwamba ifikapo Novemba 30, 2026, mradi utakuwa umekamilika,” amesema.

Aweso amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya mfano inayotekelezwa na Wizara ya Maji kwa kutumia hati fungani kama chanzo mbadala cha fedha kwa ajili ya kuimarisha huduma ya maji.

Amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na chanzo cha uhakika cha maji kitakachosaidia wananchi kupata huduma hata pale linapotokea tatizo la kiufundi au kukatika kwa umeme.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, amesema wizara itaendelea kushirikiana na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Tanga (Tanga Uwasa) katika kumsimamia mkandarasi ili kuhakikisha anatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba.

Amesema timu ya wizara itafuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo ya Waziri Aweso, huku akisisitiza kuwa ifikapo Novemba 30, 2026, miundombinu yote inayohusika na mradi inapaswa kuwa imekamilika na wananchi kuanza kupata huduma.

Mkurugenzi wa Tanga Uwasa, Geoffrey Hilly, amesema mradi huo unaendelea vizuri na umefikia wastani wa asilimia 72 kwa ujumla, huku kazi zikiendelea katika maeneo mbalimbali kuanzia chanzo hadi usambazaji wa mabomba.

Amesema mradi huo unalenga kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Tanga pamoja na Wilaya za Muheza na Mkinga, ambapo Mkinga ni miongoni mwa maeneo yatakayonufaika na maji yanayozalishwa katika mtambo wa Mowe.

Kwa mujibu wa Hilly, mradi huo unahusisha upanuzi wa mtambo wa uzalishaji maji kutoka uwezo wa kuzalisha lita milioni 45 hadi lita milioni 60 kwa siku.

Aidha, unahusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita milioni 35, litakalosaidia kuhakikisha upatikanaji wa maji wakati wa changamoto za kiufundi.

Hilly amesema tanki hilo lina uwezo wa kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi ya takribani saa 18, hatua inayotarajiwa kuongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Naye Meneja wa mradi huo kutoka kampuni ya China Railway Seventh Group, Dai Bin, ameahidi kuongeza nguvu kazi na muda wa kazi kwa kufanya shughuli za ujenzi usiku na mchana ili kuhakikisha mradi huo unakamilika ndani ya muda uliowekwa.

Amesema kampuni hiyo imepokea maelekezo ya Waziri Aweso na itayatekeleza kwa kuongeza kasi ya ujenzi ili kufikia lengo la kukamilisha mradi ifikapo Novemba 30, 2026.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment