TRAMEPRO YAWATAKA WAANDISHI KUZINGATIA WELEDI NA UHAKIKI WA TAARIFA

 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

SHIRIKA la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limewataka wananchi, viongozi, waandishi wa habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhakikisha wanahakiki taarifa kabla ya kuzisambaza, likisema taarifa sahihi ni msingi wa kujenga umoja, amani na maendeleo ya Taifa.

Wito huo umetolewa Septemba 28, 2026, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe hiyo kwa lengo la kuhamasisha upatikanaji wa taarifa, uwazi na uwajibikaji.

TRAMEPRO imesema maadhimisho hayo ni fursa ya kutafakari umuhimu wa wananchi kupata taarifa sahihi, za kuaminika, kwa wakati na zinazoweza kufikiwa, sambamba na wajibu wa kila mmoja kuzihakiki na kuzitumia kwa uadilifu.

Kwa mujibu wa shirika hilo, maendeleo ya teknolojia za kidijitali, mitandao ya kijamii na zana za akili bandia yameongeza kasi ya uzalishaji na usambazaji wa taarifa, hali inayohitaji jamii kujenga utamaduni wa kuhakiki taarifa kabla ya kuzisambaza.

TRAMEPRO imesema taarifa sahihi zina mchango mkubwa katika kujenga uelewa, kuimarisha uwajibikaji, kulinda afya ya jamii, kuhifadhi mazingira na kuimarisha umoja, amani na mshikamano wa Taifa.

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inalenga “Kulinda Uadilifu wa Taarifa katika Enzi ya Kidijitali: Nafasi ya Upatikanaji wa Taarifa katika Kukabiliana na Mkanganyiko wa Taarifa.”

Katika wito wake kwa waandishi wa habari, TRAMEPRO imewasihi kuendelea kuzingatia weledi, maadili na ukweli katika utekelezaji wa majukumu yao, huku wakihakiki taarifa kabla ya kuzichapisha.

Shirika hilo limeeleza kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu katika kujenga uelewa wa jamii na kutoa taarifa zinazoweza kusaidia kuimarisha umoja, amani na mshikamano.

Aidha, TRAMEPRO imewataka viongozi na taasisi za umma kutoa taarifa kwa wananchi kwa uwazi, usahihi na kwa wakati, huku zikitumia lugha inayoeleweka kwa jamii.

Kuhusu afya, dawa na tiba, shirika hilo limeonya dhidi ya kusambaza taarifa zisizo sahihi, likisema taarifa za aina hiyo zinaweza kuwa na madhara kwa afya na maisha ya wananchi.

Changamoto nyingine zilizotajwa ni pamoja na upatikanaji usio sawa wa teknolojia, gharama za intaneti, ujuzi mdogo wa kidijitali pamoja na ugumu wa kutambua maudhui yaliyotengenezwa au kubadilishwa kwa kutumia teknolojia ya akili bandia.

TRAMEPRO pia imewataka wataalamu wa tiba asili kuzingatia usalama, ushahidi, maadili na uwajibikaji wanapotoa taarifa kuhusu dawa na tiba asili, na kuepuka kutoa madai ya kitabibu ambayo hayawezi kuthibitishwa.

Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Mwalongo, amesema Tanzania yenye umoja na amani inahitaji utamaduni wa mawasiliano unaoheshimu ukweli na utu wa kila mwananchi.

“Taarifa sahihi hujenga uaminifu. Uaminifu hujenga uelewa na huimarisha umoja na amani,” amesema.

Ameongeza kuwa taarifa sahihi zinaweza kusaidia kuelimisha jamii kuhusu afya, kumsaidia mkulima, kumlinda mtumiaji wa dawa, kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kumwezesha mwananchi kushiriki katika maendeleo ya Taifa.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment