
Waziri Mkuu, Mwigulu Lameck Nchemba (katikati), akihutubia mamia ya Watanzania London. Wengine - kwanza kushoto Balozi wa Tanzania, Uingereza, Mbelwa Kairuki; Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa; na Mhe Angela Kairuki, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Mwanahabari mkongwe, Chama Omari Matata, aliyekuwa maarufu Radio Tanzania na BBC miaka ya Sitini hadi Tisini.
Kina dada wafanyakazi wa Benki ya NMB wakiwahudumia wanadiaspora kwa bidii
Afisa Uhamiaji Ubalozi wa Tanzania London, Ally Mtanda akizungumza na baadhi ya Watanzania washiriki. Katikati ni Maryamu Issa wa NIDA.
Na Freddy Macha, London
LONDON: Watanzania wanaoishi nchini Uingereza wamehamasishwa kutumia fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo Tanzania kwa lengo la kuchangia maendeleo ya nchi yao.
Wito huo ulitolewa wakati wa mkutano wa Tanzania Diaspora Business Forum 2026, uliohudhuriwa na Waziri Mkuu, Mwigulu Lameck Nchemba, jijini London, Uingereza, Jumapili iliyopita.
Mkutano huo wa siku moja ulifanyika katika Hoteli ya Marble Arch, magharibi mwa jiji la London, ukiwakutanisha mamia ya Watanzania waliotoka maeneo mbalimbali ya Uingereza, yakiwemo Scotland, Ireland na Wales.
Tukio hilo lililolenga kuhamasisha biashara na uwekezaji nchini lilitangazwa rasmi na Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza kupitia video iliyotolewa na Balozi Mbelwa Kairuki mwezi Septemba mwaka huu.
Kabla ya Waziri Mkuu kuhutubia mkutano huo, kulikuwa na vikao mbalimbali vilivyojadili fursa za biashara na uwekezaji nchini Tanzania, huku benki za Azania, NMB na CRDB zikishiriki kutoa taarifa kuhusu huduma zao za kifedha.
Aidha, Watanzania waliohudhuria walipata fursa ya kusajiliwa na kupata huduma za vitambulisho vya Taifa kupitia Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), zoezi lililoanza Jumamosi, Oktoba 10, na kuendelea hadi Jumapili.
Kwa mujibu wa maelezo ya mwandishi wa habari aliyeshiriki mkutano huo, hotuba zilizotolewa na viongozi kutoka Tanzania na Uingereza zilijikita katika kueleza fursa za kiuchumi zinazoweza kutumiwa na Watanzania wanaoishi nje ya nchi.
Mbali na kuwasilisha maswali na hoja zao, washiriki walipewa namba ya simu ya Waziri Mkuu kupitia WhatsApp ili waweze kuwasilisha changamoto zinazowakabili wakiwa ughaibuni. Waziri Mkuu aliahidi kujibu masuala hayo haraka iwezekanavyo.
Mkutano huo umeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na Watanzania wanaoishi nje ya nchi, pamoja na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika shughuli za biashara, uwekezaji na maendeleo ya taifa.
Kupitia mikutano ya aina hiyo, Watanzania waishio ughaibuni wanapata nafasi ya kufahamu fursa zilizopo nchini na kujadili namna wanavyoweza kutumia mitaji, ujuzi na uzoefu wao kuchangia maendeleo ya Tanzania.



0 comments:
Post a Comment