
Afande Christina Onyango, Afisa wa Polisi, mkoa wa kipolisi Ilala
akielezea namna ambavyo dawati la jinsia wamejipanga kufikisha ujumbe wa
siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini Tanzania
wakihudhuria mkutano na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa siku 16
za kupinga ukatili wa kijinsia.
Bahati Mandago kutoka shirika la Tanzania Human Rights fountain
akielezea mikakati ya shirika lake katika kufikisha ujumbe wa Funguka.
Chukua Hatua Mlinde Mtoto apate elimu.
Wadau kutoka katika mashirika mbalimbali wanaoshiriki kikamilifu
katika utekelezaji wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia wakiwa katika mkutano na waandishi wa habari
Dr.
Judith Odunga Mkurugenzi wa Shirika la WiLDAF akisoma taarifa kwa
vyombo vya habari kuhusiana na kuanza kwa siku 16 za kupinga ukatili wa
kijinsia.
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU
Katika
kuadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kuanzia tarehe 25
Novemba mpaka 10 Desemba, WiLDAF, Mashirika ya Haki za Binadamu, Wadau
wa Maendeleo na Asasi za Kiraia watatoa elimu na kuhamasisha umma
kuchukua hatua kumlinda mtoto ili apate elimu bora na salama. Ulinzi wa
mtoto ni pamoja na kuzuia vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia.
Maadhismisho
ya SIku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia mwaka huu yanalenga zaidi
kuzungumzia suala zima la usalama mashuleni, lengo kuu ikiwa
kuhamasisha umma kuhusu ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia kwa
vijana na watoto wetu mashuleni, kwani vitendo vingi vya ukatili wa
kijinsa vimekuwa vikiripotiwa.
Utafiti uliyofanywa na
Chuo cha Tiba Cha Muhimbili (MUHAS) kwa kushirikiana na Shirika la
Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika, (WiLDAF) umetambua hatari
zinazochangia ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na wazazi kutowajali
watoto na kutoa adhabu kali kwao na hivyo kuwafanya watoto kuwa na hofu.
Wakati mwingine watoto kufanyiwa ukatili bila wao kufahamu. Aidha,
adhabu ya viboko inahusishwa kama moja ya aina za ukatili dhidi ya
watoto. Hii inaathiri maendeleo ya elimu ya watoto katika taifa letu.
Kukosekana
kwa usawa kati ya watoto wa kiume na wa kike hunapelekea kuwajengea
hofu watoto wa kike, na wakati huo kuwajengea watoto wa kiume ujasiri
wa kuona kuwa ni sahihi kwao kufanya vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aidha,
tafiti kuhusu Ukatili Dhidi ya Watoto (VAC) uliofanywa na Shirika la
Umoja wa Mataifa linaloshughulikia watoto (UNICEF) wa mwaka 2011
ulionesha kwamba watoto 3 wa kike kati ya 10 na mtoto 1 kati ya watoto 7
wa kiume wenye umri kati ya miaka 13-24 wamewahi kufanyiwa ukatili wa
kingono. Aidha, asilimia 6 ya watoto wa kike wamelazimishwa kufanya
tendo la ngono kabla ya miaka 18. Pia utafiti huo unaonesha kuwa watoto
wa kike wanafanyiwa vitendo vya kingono na wanaume waliowazidi umri
wakati watoto wa kiume wanafanyiwa ukatili na watoto wenye umri sawa.
Tafiti
pia imeonesha kuwa vitendo hivyo vinafanywa na watu wanaowafahamu
wakiwemo majirani, wapenzi wao, watu wenye mamlaka (walimu). Ni
asilimia 32.2 tu ya watoto wa kike na asilimia 16.6 ya watoto wa kiume
wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na watu wasiofahamika na
watoto. Vitendo hivi hufanyika maeneo ambayo uangalizi wa watu wazima
unahitajika kuwepo kwa mfano mashuleni, njiani, majumbani na wakati
mwingine katika vyombo vya usafiri.
Ni dhahiri kwamba
kwa mazingira, mila na utamaduni ikijumuisha familia za Kitanzania,
vimekuwa vikichangia vitendo vya ukatili wa kijinsia. Vitendo vya
ukatili na udhalilishaji vina madhara makubwa ya kiafya kwa watoto kwani
hukatisha uwezo wao wa kielimu, mahudhurio ya shule na hivyo kupelekea
matokeo mabaya ya katika ufaulu wao wakati wa mitihani.
Aidha,
mazingira yasiyo salama kwa watoto wa shule yana madhara makubwa.
Watoto wanapokuwa mashuleni na kufanyiwa ukatili wa kingono wapo katika
hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi ya UKIMWI kwa mathlani mara tatu
zaidi ya wale ambao hawajawahi kufanyiwa ukatili.
Tunaamini
kwamba kuondolewa kwa vikwazo vinavyo chochea ukatili wa kijinsia kwa
watoto wa shule kutachangia katika kuleta usawa wa kijinsia kwa watoto
wa kiume na wa kike. Pia mazingira mazuri ya shule yatasaidia mahudhurio
mazuri ya watoto mashuleni na kuleta matokeo mazuri katika ufaulu.
Jamii
inahaswa kuweka mazingira mazuri ya shule ikiwa ni pamoja na kuwepo
miundombinu kama mabweni, vyoo, madawati, uzio kuzunguka mashule na
vyombo rafiki vya usafiri. Haya yote yatawezekana tu ikiwa kutakuwa na
dhamira ya dhati kwa watunga sera, wazazi, walimu, wanafunzi na jamii
kwa ujumla katika kuzuia ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto.
Kuna haja ya makusudi kabisakutofumbia macho masuala ya ukatili kwa
ujumla wake ili kujenga jamii imara
Siku 16 za Kupinga
ukatili wa kijinsia ni tukio la kimataifa la kila mwaka ili kuwa na
nguvu ya pamoja katika kuzuia kuenea kwa janga hili . Ndani ya siku
hizi, kuna siku zingine muhimu za kimataifa , mathlani, Novemba 25 ni
Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake, Novemba 29 ni
Siku ya Kimataifa ya Watetezi wa Haki za Binadamu, Desemba 1 ni Siku ya
UKIMWI Duniani, Desemba 3 ni Siku ya Kimataifa ya watu wenye Ulemavu,
Desemba 6 ni Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Mauaji ya kikatili ya
Montreal 1989, ambapo wanawake 14 waliuawa na mtu aliyekuwa anawachukia
wanawake. Tarehe hizi zilichaguliwa mahususi ili kuhusianisha kwamba
ukatili wa kijinsia unaongeza maambukizi ya UKIMWI na ni Ukiukwaji wa
Haki za Binadamu.
Katika kipindi hiki cha Kampeni ya
Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia , mamia ya asasi za kiraia na
wadau mbalimbali Tanzania wataifikia jamii kwa kauli mbiu inayosema;
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.
Kauli hii
inalenga kumshawishi mtu binafsi, kuwashawishi walimu, wanafunzi, wazazi
na jamii kwa ujumla, kuwalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia na
kuhakikisha kwamba shule ni mahala salama. Ni vema kutafakari kwa kina
jinsi vitendo vya ukatili wa kijinsia mashuleni vinavyoathiri maendeleo
ya watoto wetu kielimu. Hivyo na haja ya kuwa na taifa linalopiga vita
vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Taifa linalofumbia macho ukatili
wa kijinsia haliwezi kupiga hatua kimaendeleo.
Kampeni
ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia ina lengo la kushawishi
watunga sera, wadau na jamii kwa ujumla, kuchukua hatua dhidi ya ukatili
wa kijinsia . Pia ina taka jamii kufichua vitendo vyote vya ukatili wa
kijinsia ili kuwa na jamii isiyovumilia ukatili wa aina yoyote.
Hivyo basi WiLDAF na wadau mbalimbali wanaopinga vitendo vya ukatili wa kijinsia wanaitaka serikali kufanya yafuatayo;
1) Kufutwa kwa adhabu ya viboko mashuleni na walimu kutafuta mbinu za kutoa adhabu mbadala.
2)
Kutengeneza muongozo wa utekelezaji wa sera ya elimu ya mwaka 2014
utakaolekeza upatikanaji wa elimu ya msingi iliyo bora na salama.
3)
Kuboresha miundo mbinu rafiki kwa watoto wa shule ikiwa ni pamoja na
kuwepo kwa vyoo bora, mabweni, madawati, usafiri, uzio kuzunguka shule
na mengineyo kwa ustawi wa watoto wa shule.
4) Kuunda mabaraza yatakayokuwa yanasimamia malalamiko ya wanafunzi mashuleni.
5)
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikiana na Wizara ya
sheria na Katiba zitunge sheria ya kudhibiti Ukatili Majumbani na
kubadilisha Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971inayoruhusu mtoto wa kike chini
ya miaka 18 kuolewa, ama kwa ridhaa ya wazazi, mlezi au Mahakama.
Katika
kipindi hiki cha siku 16, za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na
shughuli mbalimbali na midahalo ili kuleta mabadiliko katika nchi yetu.
Tunatoa wito kwa jamii kwa ujumla kupaza sauti na kukemea vitendo vyote
vya ukatili wa kijinsia. Jamii ihamasishe usawa wa kijinsia, mahusiano
yasiyo na ukatili na isibague au kunyanyapaa waathirika wa ukatili wa
kijinsia. Tusikae kimya bali tufichue ukatili wa kijinsia na kuchukua
hatua kuwalinda watoto wetu iliwapate elimu bora na iliyo salama. Kwa
pamoja kupitia kauli mbiu ya mwaka tunasisitiza;
FUNGUKA! CHUKUA HATUA MLINDE MTOTO APATE ELIMU.
0 comments:
Post a Comment