Na Tumaini Msowoya, Dar es Salaam.
Naibu
Waziri wa Elimu, Stella Manyanya (pichani) amesema, mpango wa Serikali wa kutoa
elimu bure kuanzia darasa la kwanza hadi Kidato cha Nne hauwaondolei
wazazi majukumu ya msingi kuhakikisha watoto wanapata elimu bora.
Akizungumza
na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Manyanya (pichani) alisema sera
ya elimu bure inalenga kuwapunguzia mzigo wazazi hasa wa gharama kama
ada ambazo awali walikuwa wakilipa serikalini.
“Nadhani
watu hawajaelewa. Zamani elimu ilikuwa ikitolewa kwa ubia kati ya
Serikali na mzazi, kila upande una jukumu la kufanya kwa ajili ya elimu
ya mtoto. Serikali ilikuwa inamlipa mwalimu na kukusanya Sh20,000 kwa
wanafunzi wa kutwa na Sh70,000 kwa wanafunzi wa bweni,” alisema na
kuongeza kuwa:
“Tuliposema elimu bure, maana yake sasa
ile Sh 20,000 na Sh 70,000 zilizokuwa zinakusanywa na Serikali, tumesema
sasa mzazi asitoe tena na hiyo imesaidia sana maeneo ya vijijini ambako
wazazi walishindwa kulipa ada hiyo. Haikumaanisha kwamba sasa mzazi
asiwe na jukumu kabisa katika elimu ya mtoto wake.”
Manyanya
alisema itashangaza kama kuna wazazi ambao hawatawajibika kwa masuala
ya msingi kabisa ya mtoto kupata elimu wakiitegemea Serikali kufanya
kila kitu.
“Kama shule haina madawati, watoto wanakaa chini na wazazi wako tayari kuchangia, kwa nini wasichangie” alihoji Manyanya.
Dhana
ya elimu bure ambayo utekelezaji wake unasimamiwa na Ofisi ya Rais
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inazingatia uendeshaji wa shule
bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi ama
walezi.
Dhana hii ni utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.
Elimu bora
Wakati
dhana ya elimu bure ikiendana na ubora wa elimu hasa kukuza kiwango cha
ufaulu, Manyanya alisema Serikali imeanza mchakato wa kuwakagua
wakaguzi wa shule na kuwabana wasiotekeleza wajibu wao ipasavyo.
Pia
aliwatangazia kiama baadhi ya walimu wanaozembea kufundisha kwa
kisingizio cha kulipwa mishahara midogo, jambo linalochangia kushuka kwa
kiwango cha elimu nchini.
Alisema Serikali
haitawavumilia walimu na wakaguzi wa aina hiyo na kwamba wanaandaa
mapendekezo ya kubadilisha baadhi ya sheria zinazoruhusu mlolongo mrefu
wa namna ya kuwashughulikia kinidhamu watumishi.
“ Kama
wakaguzi watafanya kazi kwa ufasaha, watagundua na kuvumbua
yanayofanyika shuleni, kwa hakika kiwango cha elimu kitaongezeka. Idara
hii ikiyumba, elimu nayo itayumba,” alisema.
Alisema
kila mkaguzi atatakiwa kutoa taarifa ya ukaguzi wake na kufanyiwa kazi
kwa kiwango cha juu ili kujiridhisha kama ina uhalisia na kama italeta
mabadiliko.
Kuhusu walimu, Mhandisi Manyanya alisema
wapo walimu wachache wazembe na wasiotekeleza wajibu wao kwa maksudi
wakilalamikia kuwa mishahara ni midogo.
“Ni vibaya na
hatari kupokea mshahara ambao unausema mdogo na kwa sababu hiyo hutaki
kufundisha, kuna walimu wengi hawajaajiriwa na ikiwa unaona haukutoshi
ni vizuri ukawapisha wenzako,” alisema na kuongeza;
“Hakuna
kitu kibaya kama kudharau na kutoheshimu kazi yao eti kwa kuwa unalipwa
kidogo; ukiona darasa unalofundisha wanafunzi hawakuelewi na mitihani
yako wanafeli, jiulize mara mbili,”alisema.
0 comments:
Post a Comment