CHINA KUTOA UFADHILI WA MASOMO MAKAA YA MAWE

Teresia Mhagama na Zuena Msuya.
Imeelezwa kuwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China itatoa ufadhili wa masomo kwa watanzania ili  kujifunza masuala ya makaa ya mawe kupitia Vyuo mbalimbali vya nchi hiyo ili kuongeza idadi ya  wataalam hao nchini.

Hayo yameelezwa jijini Dar es Salaam na Balozi China nchini Tanzania Dkt.Lu Youqing wakati  wa kikao chake na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kilicholenga katika kujadili uendelezaji wa makaa mawe nchini ambayo ni moja ya chanzo cha uzalishaji umeme.

Katika kikao hicho Dkt. Youqing aliambatana na watendaji wa Serikali na  kampuni mbalimbali zinazojishughulisha na uendelezaji  wa makaa ya mawe ikiwemo kuzalisha umeme katika Jimbo linalojitegemea la Ningxia ambalo lipo nchini China.

“ Mwaka ujao tutatoa ufadhili wa masomo kwa watanzania 10 hadi 15 kujifunza masuala ya makaa ya mawe nchini China pia tutatoa ufadhili wa mafunzo ya muda mfupi kwa wataalam waliopo kazini  na  Serikali ya Watu wa China itagharamia kila kitu,” alisema Dkt. Lu Youqing.

Balozi huyo wa China alisema hayo baada ya Profesa Muhongo kumueleza kuwa nchi ina uhaba wa wataalam waliobobea katika masuala ya makaa ya mawe kwani hadi sasa yupo mtaalam mbobezi mmoja ambaye naye anakaribia kustaafu.

“Tulikuwa na mtaalam ambaye amekwishastaafu na sasa tumebakiwa na mmoja katika Wakala wa Jiolojia Tanzania, hivyo ombi langu kuu ni kuendeleza watanzania katika sekta hiyo ili tuwe na wataalam wa kutosha,  hivyo mwakani naomba mtusaidie kuwasomesha watanzania  10 hadi 20 na pia kutoa mafuzo ya muda mfupi kwa wahandisi na wajiolojia ambao tayari wapo kazini,” alisema Profesa Muhongo.

Aidha Profesa Muhongo alimsisitiza Balozi wa China nchini kuhakikisha kuwa maombi hayo ya mafunzo ya  makaa ya mawe hayaathiri nafasi 20 za Ufadhili wa masomo ya Shahada za Uzamili na Uzamivu  katika Sekta ndogo ya Mafuta na Gesi ambazo Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China imepanga kutoa.

Akizungumzia mashirikiano yanayoweza kufanyika kati ya Serikali ya Tanzania na Jimbo la Ningxia, Profesa Muhongo aliwakaribisha watendaji wa Serikali hiyo na makampuni ya nchi hiyo kushirikiana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) ili kuiwezesha maabara ya Wakala huo kuwa yenye teknolojia ya kisasa itakayowezesha kutambua aina ya makaa ya mawe yaliyopo nchini pamoja na kuwa na takwimu sahihi za mashapo ya madini hayo.

“ Takwimu za mashapo ya makaa ya mawe tunazozitoa sasa zimekuwa za kukadiria hivyo tunahitaji mshirikiane na GST kushughulikia suala hilo ili tuwe na takwimu sahihi za madini hayo,” alisema Profesa Muhongo.

Suala lingine alilosisitiza kwa makampuni hayo ya  Ningxia ni kuwekeza katika uendelezaji wa mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambapo mashapo yaliyopo katika mgodi huo yanaweza kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 200 hadi 300 na kueleza kuwa Serikali haitatoa mgodi huo kwa kampuni zisizokuwa na fedha wala teknolojia ambazo zinataka kuutumia mgodi huo kupata fedha kwa mahitaji binafsi ya kampuni hizo.

Kwa upande wake Mwakilishi Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Biashara kutoka Jimbo la Ningxia, Li Zighong, alisema kuwa Serikali ya Jimbo hilo imeamua kuwa na Ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika uendelezaji wa makaa ya mawe kwani Tanzania ni moja ya nchi barani Afrika ambayo ina sera nzuri zinazoongoza sekta mbalimbali  na hivyo kupelekea ukuaji wa kiuchumi na kiteknolojia.

Alisema kuwa Jimbo hilo la Ningxia linashika nafasi ya 6 nchini China kwa kuwa na wingi wa mashapo ya makaa ya mawe na wana  uzoefu wa uzalishaji umeme unaotokana na nishati hiyo. 
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akiwa na Mwakilishi Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Biashara kutoka Jimbo linalojitegemea la Ningxia nchini China,  Li Zighong (kushoto) katika mkutano uliolenga kuendeleza madini ya makaa ya mawe nchini ili yaweze kuzalisha nishati ya umeme.Kikao kilifanyika katika Makao Makuu ya Wizara ya Nishati na Madini jijini  Dar es Salaam.
 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akiwa na Mwakilishi Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Biashara kutoka Jimbo linalojitegemea la Ningxia nchini China,  Li Zighong (anayetia saini) pamoja na Balozi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Dkt.Lu Youqing mara baada ya kumaliza mkutano uliolenga kuendeleza madini ya makaa ya mawe nchini.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ( katikati) akiongoza kikao kilichojumuisha watendaji wa makampuni yanayojighulisha na  Makaa ya Mawe  kutoka Jimbo linalojitegemea la Ningxia nchini China, Watendaji wa Ubalozi wa  Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake. Kikao hicho kililenga kujadili masuala mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa umeme wa makaa ya mawe yaliyopo nchini. Kushoto kwa Waziri ni Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe na kulia kwa Waziri ni Mwakilishi Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Biashara kutoka Jimbo linalojitegemea la Ningxia nchini China,  Li Zighong. 

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (Wa Pili kulia) akiwa na Mwakilishi Mkuu wa Masuala ya Uchumi na Biashara kutoka Jimbo linalojitegemea la Ningxia nchini China,  Li Zighong (wa Pili kushoto) pamoja na Balozi wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Dkt.Lu Youqing (wa kwanza kulia) wakiwa wameshikilia picha yenye ujumbe wa kuusifu ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali za Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China ambayo waliikabidhi kwa Profesa Muhongo mara baada ya kumaliza mkutano uliolenga kuendeleza madini ya makaa ya mawe nchini ili yaweze kuzalisha nishati ya umeme.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment