BENKI YA POSTA TANZANIA, YASAIDIA SHULE ZA MSINGI WILAYANI ILEJE MKOANI MBEYA

  Naibu waziri wa Viwanda na Biashara, Janet Mmbene, (wapili kushoto), akipeana mikono na Meneja msaidizi wa Benki ya Posta Tanzania, TPB, tawi la Tunduma, Teddy Msanzi, wakati wa hafla ya kukabidhi madawati yaliyotolewa kama msaada na benki hiyo, kusaidia shule mbili za msingi wilayani Ileje, mkoa wa Mbeya, hivi karibuni

NA K-VIS MEDIA
Benki ya Posta Tanzania (TPB) kupitia tawi lake la Tunduma, imetoa msaada wa madawati 100 yenye thamani ya shilingi Milioni Tatu kwa shule mbili za Msingi zilizopo Wilayani Ileje, mkoani Mbeya.

Akikabidhi madawati hayo kwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Janeth Mbene kwenye hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika Wilayani humo hivi karibuni, Meneja wa Benki ya Posta Tawi la Tunduma Teddy Msanzi alisema kuwa,  Benki yake iliguswa sana na suala la uhaba wa madawati kwa wanafunzi wa Wilaya hiyo na kuona ni muhimu kusaidia.

“Benki ya Posta inatambua umuhimu wa elimu bora kwa ajili ya kujenga kizazi bora cha baadae. Ni vigumu kutoa elimu bora katika mazingira magumu ya wanafunzi kukaa chini madarasani.Ni vema wanafunzi wetu wakawekewa mazingira mazuri ya kupata elimu, ikiwemo madawati. 

Hivyo basi sisi Benki ya Posta tunatoa madawati haya 100 ili kupunguza tatizo hili.” Alifafanua Teddy.

Kwa mujibu wa taarifa ya ofisi ya elimu wilaya Ileje, Wilaya hiyo ina jumla ya wanafunzi 28,488 wa shule za Msingi , lakini idadi ya madawatii ni 10,028, na kufanya idadi ya madawati yanayohitajika kuwa 4,116.

Akitoa shukrani zake kwa niaba ya shule za Wilaya ya Ileje, Mhe. Janeth Mbene aliishukuru Benki ya Posta kwa msaada huo ambao alisema ni mkombozi kwa wanafunzi waliokuwa wakikaa chini kwa muda mrefu. Alitumia fursa hiyo pia kuziomba taasisi nyingine ziguswe na tatizo lao na ziweze kuwasaidia ili waweze kuondokana na changamoto hiyo.
 Naibu Waziri Mmbene, akiwa na maafisa wa benki hiyo, tawi la Tunduma
 Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Janet Mbene akimkabidhi katibu wa CCM Wilaya ya Ileje Hamida Mbogo madawati ya kwa ajili ya shule za sekondari na msingi wilayani ileje ambayo yametolewa na benki Posta Tawi la Tunduma.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment