Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu mpango aliouanzisha wa walimu kutotoa nauli kwenye daladala wakati wa kwenda na kurudi nyumbani wanapotoka kazini. Kushoto ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DACOBOA), Sabri Mabrouke.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DACOBOA), Sabri Mabrouke (kushoto), akizungumzia mpango huo ambao wameuunga mkono. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU), Shaban Mdemu, Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam (DACOBOA), William Masanja.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wasafirishaji Abiria Dar es Salaam (DACOBOA), William Masanja (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Madereva Tanzania (TADWU), Shaban Mdemu (kulia), akizungumza katika mkutano huo.
Taswira ya meza kuu katika mkutano huo.
Mwonekano wa meza kuu katika mkutano huo.
Mkutano na wanahabari ukiendelea.
............................................................
Taarifa kwa Umma kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda.
Moja ya jambo
ambalo serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa John
Pombe Magufuri imelifanya kuwa kipaumbele kikubwa kwenye mipango yake ya kimaendeleo
ni suala la uboreshaji wa sekta ya elimu nchini na ndio maana serikali imeanza
utekelezaji wa mpango huu kwa kufuta ada zote mashuleni.
Kimsingi ni
ndoto hii ya Mheshimiwa Raisi ambayo nina hakika kila mmoja wetu anaelewa
ukubwa wa faida zake kwenye ujenzi wa Tanzania mpya na yenye wasomi na
wataalamu wa kila namna tena wanaopatikana bila kuzingatia hali ya kipato cha
familia anayotokea mwanafunzi, iliyonifanya mimi kama msaidizi wake katika
nafasi ya ukuu wa wilaya nijiulize kila wakati juu ya ushiriki wangu wa
kuhakikisha inatimia kikamilifu.
Maswali ambayo yamenifikisha kwenye wazo la kuboresha
sekta hii kwa kuchagua kufanya jambo ambalo wakati serikali ikiendelea
kupigania changamoto nyinginezo za kuboresha ajira za walimu ikiwemo upandishwaji
wa madaraja na mishahara, basi na mimi katika nafasi yangu nishiriki kwenye mchakato
huu mzima kwa kutoa motisha ya usafiri wa bure kwa walimu wote wanaofundisha kwenye
shule za serikali zilizopo jijini Dar es Salaam.
Kwa ufupi ni
kwamba, wazo hili limejengwa juu ya msingi wa sababu kubwa tatu.
Moja, kwa
kuzingatia changamoto za nauli za mara kwa mara wanazolazimika kuzilipa walimu
ili kuyafikia kwa wakati maeneo yao ya kufanyia kazi na pili, ni kuhakikisha
mimi na serikali yangu ya wilaya ya Kinondoni tunakuwa sehemu ya juhudi za
Mheshimiwa Raisi za kuboresha maslahi na mazingira ya walimu ya kufanyia kazi
ili matarajio ya ndoto yake anayoipigania usiku na mchana ya kutaka kuiona
sekta ya elimu nchini ikikua kwa kasi yanatimia.
Na tatu, ni kuwafanya walimu wa
wilaya ya Kinondoni na Dar es Salaam kwa ujumla kama watumishi wenzangu wa
serikali nao wanafaidi sehemu ya matunda ya serikali yao ambayo kwa dhati
imedhamiria kubadilisha maisha yao ili na wao waweze kubadilisha maisha ya
vijana wetu kupitia taaluma.
Kwasababu hizo
nilizozianisha hapo juu ninaomba kuwatangazia walimu wangu wa shule zote za serikali
kuanzia za msingi mpaka sekondari ya kwamba, sasa watasafiri bure wanapokwenda
kutufundishia wadogo zetu na watoto wao.
Hii ni baada ya kufanya vikao na mazungumzo
ya kina na wamiliki wa vyombo vya usafiri wa umma kupitia vyama vyao vya
Darcoboa na Uwadar na hatimaye mazungumzo hayo kuitimishwa na mkutano wa vyama vyote
hivyo viwili vya wamiliki wa vyombo vya usafiri ambao kwa sauti moja wamekubali
kuniunga mkono kwenye utekelezaji wa wazo langu hili.
Kipekee na kwa
unyenyekevu mkubwa, naomba kuchukua fursa hii kuwashukuru sana wamiliki hawa wa
vyombo vya usafiri wa umma pamoja na viongozi wa vyama vya Darcoboa na Uwadar
kwani walikuwa na kila sababu ya kukataa hasa ukizingatia kuwa wao ni
wafanyabiashara na tena wanazo changamoto nyingi katika sekta yao ya usafirishaji,
wengine wakiwa hata wamekopa kwenye mabenki ili wapate uwezo wa kufanya
biashara, lakini kwenye jambo hili wote kwa umoja wao wameseme ndio na wako
tayari kuanza haraka iwezekanavyo.
Utaratibu kwa
walimu juu ya utumiaji wa fursa ambayo tumeipata utakuwa kama ifuatavyo:- Moja,
nimemuelekeza ofisa elimu wa sekondari na shule za msingi, kutoa maelekezo kwa
wakuu wa shule zote za serikali zilizopo wilayani kwangu na wilaya nyinginezo
za jiji la Dar es Salaam, kutengeneza vitambulisho vya shule zao vitakavyokuwa
na picha ya mwalimu, jina lake kamili, jina la shule anayofundisha, namba ya
simu ya mkuu wa shule husika pamoja na saini yangu mimi mwenyewe Paul Makonda
ili kuepuka udanganyifu.
Nimewataka zoezi
hili walifanye na kulikamilisha ndani ya wiki moja ambapo baada tu ya
kukamilika itakuwa ni furaha yangu kuwatangazia walimu wote wa shule za
serikali jijini Dar es Salaam kuwa, watakuwa wakipanda daladala bure ila tu kwa
siku za jumatatu mpaka Ijumaa na kwa muda wa saa kumi na moja asubuhi mpaka saa
mbili asubuhi na kati ya saa tisa mpaka saa kumi na mbili jioni. Ingawa, kila
mwalimu atalazimika kuonyesha kitambulisho chake alichotengenezewa kwenye shule
yake pamoja na kile cha ajira ya serikali.
0 comments:
Post a Comment