FCC Yaimarisha Mapambano Dhidi ya Bidhaa Feki, Yasisitiza Ushindani wa Haki Sokoni

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, akizungumza wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyoandaliwa na Tume hiyo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, Februari 24, 2026.
Makamu wa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Habari Mkoa wa Dar ea Salaam (DARPC) Mary Geofrey akitoa maelezo kuhusiana na semina ya FCC itavyochochea ushindani wa soko ,jijini Dar es Salaam.
Semanina ikiendelea 
Picha pamoja ya wafanyakazi wa FCC na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa katika Semina ya Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.
Picha pamoja ya waandishi wa Habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC Khadija Ngasongwa katika Semina ya Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.



Dar es Salaam — Tume ya Ushindani nchini, Fair Competition Commission (FCC), imesema itaendelea na mchakato wa marekebisho ya sheria zake ili kuimarisha ulinzi wa walaji, kudhibiti bidhaa bandia na kuhakikisha kunakuwepo ushindani wa haki unaochochea ukuaji wa uchumi na ajira.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, wakati akifungua semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Ngasongwa alisema marekebisho hayo yanalenga kumlinda mlaji dhidi ya bidhaa zisizo na ubora, matangazo ya upotoshaji pamoja na vitendo vinavyokiuka misingi ya ushindani wa haki sokoni.

Alibainisha kuwa moja ya vipaumbele vya tume hiyo ni kuimarisha udhibiti wa bidhaa bandia zinazoingia nchini, akieleza kuwa bidhaa hizo huathiri afya za wananchi, hupunguza mapato ya Serikali na kuwanyima wafanyabiashara halali fursa ya kukuza biashara zao.

“Jukumu letu ni kuhakikisha uchumi unakua kwa misingi ya ushindani wa haki, jambo linalochochea uwekezaji na kuongeza ajira kwa wananchi,” alisema.

Aidha, FCC imesema itaendelea kukutana mara kwa mara na waandishi wa habari pamoja na wadau mbalimbali ili kutoa taarifa sahihi kuhusu majukumu yake na kusikiliza changamoto za wananchi kwa lengo la kuzitatua kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Ngasongwa alisema kuna maboresho yanayoendelea kupitia mfumo wa TANOGA, unaojumuisha taasisi za udhibiti na mawakala wa forodha, kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa bidhaa zinazoingia nchini.

Aliongeza kuwa taasisi hizo zinaelekea kuingia katika mfumo wa kidijitali utakaopunguza mwingiliano wa moja kwa moja kati ya watumishi na wateja, hatua itakayosaidia kuongeza uwazi, kupunguza urasimu na kudhibiti mianya ya vitendo visivyo vya kiadilifu.

FCC imeahidi kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali pamoja na sekta binafsi ili kuhakikisha mazingira ya biashara nchini yanabaki kuwa salama, yenye ushindani wa haki na yenye manufaa kwa wananchi.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment