Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete aweka saini kitabu cha maombolezo cha Marehemu Kardinali Pengo

Na Mwandishi Wetu.

Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, leo ameweka saini katika kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Katoliki la Dar es Salaam, marehemu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu jijini Dar es Salaam.

Baada ya kuweka saini, Dkt Kikwete alimpa mkono wa pole Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Thaddaeus S. Ruwa’ichi, na kueleza kuwa marehemu Kardinali Pengo atakumbukwa daima kwa mchango wake mkubwa kwa Kanisa na Taifa pamoja na moyo wake wa upendo kwa wananchi na kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema Kardinali Pengo alikuwa rafiki wa wengi na kiongozi aliyegusa maisha ya watu wengi kupitia huduma yake ya kiroho na kijamii.

Aidha, Dkt Kikwete alitoa pole kwa Askofu Mkuu Ruwa’ichi, viongozi na waumini wa Kanisa Katoliki, akiwataka kuwa na subira katika kipindi hiki cha majonzi huku akiungana nao kumuombea marehemu apumzike kwa amani.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa pole, Rais huyo Mstaafu alisema yeye na marehemu Kardinali Pengo walifahamiana kwa muda mrefu tangu alipokuwa akihudumu wilayani Nachingwea katika kituo chake cha kwanza cha kazi, wakati marehemu akiwa Askofu Mkuu aliyesimamia maeneo ya Tunduru na Lindi.

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Thaddaeus S. Ruwa’ichi, alitangaza msiba huo tarehe 19 Februari 2026 saa 04:00 kwa masikitiko makubwa, akieleza kuwa mpendwa baba yetu, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, ameitwa nyumbani kwa Baba wa Milele akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa ratiba rasmi ya mazishi, shughuli za kuaga mwili wa marehemu zitaanza siku ya Jumamosi tarehe 28 Februari 2026 kwa kuwasili kwa mwili katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu saa 03:00 asubuhi.

Kuanzia saa 03:15 asubuhi hadi saa 10:00 jioni waombolezaji watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu.
Saa 10:00 jioni kutakuwa na Misa Takatifu ya kumuombea marehemu itakayofuatiwa na mkesha wa sala na maombolezo utakaoshirikisha makundi mbalimbali ya kijimbo, wakiwemo watawa, walei pamoja na vyama vya kitume.

Siku inayofuata, yaani Jumapili, mwili wa marehemu utaondoka Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu saa 12:00 asubuhi kuelekea Kituo cha Hija Pugu, na unatarajiwa kuwasili saa 12:45 asubuhi chini ya usimamizi wa Kamati ya Mazishi.

Kuanzia saa 01:00 hadi saa 03:45 asubuhi waombolezaji watapata tena fursa ya kutoa heshima za mwisho katika Kituo cha Hija Pugu.

Misa ya Mazishi itaanza saa 04:00 asubuhi katika Kituo cha Hija Pugu, ikihitimisha rasmi shughuli za mazishi.

Waumini na wananchi wote wanaombwa kushiriki katika ibada na sala hizi kwa utulivu na heshima inayostahili.
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa tarehe 5 Agosti 1944 na kupadrishwa mwaka 1971.

Alisoma Teolojia ya Maadili katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Lateran mjini Roma, ambako alipata shahada ya uzamivu mwaka 1977. Baadaye alifundisha katika Seminari ya Kipalapala na kuwa Rektor wa kwanza wa Seminari ya Segerea hadi mwaka 1983.

Aliteuliwa kuwa Askofu wa Nachingwea mwaka 1983 na baadaye Askofu wa Jimbo la Tunduru–Masasi mwaka 1985. Mwaka 1990 aliteuliwa kuwa Askofu Mkuu Msaidizi wa Dar es Salaam na mwaka 1992 akawa Askofu Mkuu kamili wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

Mwaka 1998 alitangazwa kuwa Kardinali na Papa Yohane Paulo II, na alishiriki katika mikutano ya kumchagua Papa mwaka 2005 na 2013.

Kardinali Pengo alihudumu pia katika idara mbalimbali za Kanisa Katoliki la Roma na kuongoza Baraza la Makanisa Katoliki Afrika (SECAM) tangu mwaka 2007. Alistaafu mwaka 2019, akiacha alama ya uongozi thabiti na imani isiyotetereka.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment