Serikali yaweka mkakati wa kuitangaza Tanzanite na madini ya vito nchini Qatar

Na Mwandishi Wetu, Doha

Serikali ya Tanzania imeanza mkakati mpya wa kimataifa wa kutangaza madini ya Tanzanite katika soko la Mashariki ya Kati, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kurejesha hadhi na thamani ya madini hayo adimu duniani.

Akizungumza Februari 25, 2026 jijini Doha, Waziri wa Madini Anthony Mavunde alisema serikali imeamua kuongeza juhudi za kuitangaza Tanzanite kimataifa baada ya kubaini kuwa baadhi ya masoko bado hayafahamu asili ya madini hayo kuwa yanapatikana Tanzania pekee.

Alisema kushuka kwa uelewa wa soko la kimataifa kumeathiri bei na mauzo ya madini hayo, hivyo wizara imeanza hatua za kuyafikia masoko mapya na kuwavutia wawekezaji pamoja na wafanyabiashara wa vito.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alitembelea Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar ambapo alikutana na watumishi wa ubalozi na kukubaliana kuandaa mkutano wa wawekezaji na wafanyabiashara wa madini kati ya nchi hizo mbili.

Aidha, serikali imepanga kuratibu ushiriki wa wafanyabiashara wa madini ya vito kutoka Tanzania katika maonesho ya kimataifa ya madini yatakayofanyika Doha mwezi Aprili 2026, yakilenga kupanua masoko, kuongeza uwekezaji na kuimarisha utalii unaotokana na rasilimali madini.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mheshimiwa Habibu Awesi Mohamed, alisema fursa za ushirikiano katika sekta ya madini ni kubwa na zikiendelezwa zinaweza kuongeza mapato ya taifa na kukuza uchumi

Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati mpana wa serikali wa kuitangaza Tanzanite kama alama ya kipekee ya Tanzania duniani na kuongeza mcvhango wa sekta ya madini katika uchumi wa taifa.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment