Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM — Taasisi ya Heart Team Africa Foundation (HTAF) kwa kushirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), imezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya “Kutoa Ni Moyo” yenye lengo la kuchangisha fedha na kuongeza uelewa kwa ajili ya kusaidia watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo nchini.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa Mei 25, 2026 jijini Dar es Salaam inalenga kuwaunganisha Watanzania kutoka sehemu mbalimbali za jamii ili kuwapa watoto wanaozaliwa na matatizo ya moyo nafasi ya kupata matibabu na huduma muhimu za moyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge alisema zaidi ya watoto 16,000 huzaliwa kila mwaka nchini Tanzania wakiwa na matatizo ya moyo, hali inayozifanya familia nyingi kukumbana na changamoto kubwa za kiafya na kifedha.
Alisema takribani watoto 4,000 wanahitaji upasuaji wa moyo kwa haraka, huku akibainisha kuwa kwa familia nyingi muda si suala la fedha pekee bali ni suala la kuokoa maisha.
"Kupitia kampeni ya Kutoa Ni Moyo, tunatoa wito kwa Watanzania wote, taasisi, makampuni binafsi pamoja na taasisi za serikali kuwa sehemu ya harakati hizi za kuokoa maisha ya watoto," alisema Dkt. Kisenge.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HTAF, Dkt. Naizihijwa Majani alisema kampeni hiyo imekusudia si tu kukusanya fedha, bali pia kujenga uelewa wa muda mrefu kuhusu afya ya moyo na umuhimu wa jamii kushiriki kusaidia.
Alisema Tanzania ina utamaduni mkubwa wa mshikamano na kusaidiana, hivyo kampeni hiyo inalenga kubadili michango midogo ya wananchi kuwa nguvu kubwa ya kitaifa yenye matokeo makubwa.
"Hii si kampeni ya kuchangisha fedha pekee, ni harakati inayojengwa juu ya huruma, umoja na imani kuwa kuokoa maisha ya mtoto ni jukumu la kila mmoja wetu," alisema Dkt. Majani.
Takwimu zinaonyesha kuwa magonjwa ya moyo husababisha vifo vya watu milioni 17.9 duniani kila mwaka, huku mtoto mmoja kati ya watoto 100 akizaliwa akiwa na tatizo la moyo.
Kampeni hiyo inalenga kukusanya shilingi bilioni 25 kupitia michango ya wananchi, makampuni, wadau wa maendeleo, taasisi mbalimbali, Watanzania waishio nje ya nchi, watu maarufu, jumuiya za michezo na jamii kwa ujumla.

Fedha zitakazokusanywa zitatumika kugharamia upasuaji na matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, uchunguzi wa mapema, programu za elimu ya afya ya moyo pamoja na kusaidia familia zinazokabiliwa na changamoto hiyo.
Aidha, kampeni hiyo itatumia mifumo ya kidijitali na majukwaa ya uchangishaji mtandaoni ili kurahisisha Watanzania kuchangia kwa uwazi na urahisi kutoka ndani na nje ya nchi.
Taarifa zinaonyesha kuwa juhudi za awali za uchangishaji tayari zimefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 3.08 kupitia fedha taslimu na misaada ya vifaa mbalimbali.
0 comments:
Post a Comment