Na Mwandishi Wetu. Mwenyekiti wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Tido
Mhando, amewataka Waandishi wa Habari nchini kutafakari upya wajibu wao
katika kuijenga jamii kupitia maudhui yenye tija, akieleza kuwa ipo haja
ya kurejesha hadhi na nguvu ya taaluma hiyo katika kujenga fikra na
maendeleo ya taifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Bw. Mhando
amesema pamoja na JAB kusimamia utoaji wa ithibati kwa kuzingatia vigezo
vya elimu na sheria, bado kuna umuhimu wa Waandishi wa Habari kuendelea
kujengewa uwezo kupitia mafunzo ya kitaaluma.
“Tukitazama baadhi
ya vyombo vyetu vya habari, iwe ni magazeti, redio au televisheni,
mambo ya kufikirisha kwa kiasi kikubwa yamepungua. Waandishi wa Habari
wanapaswa kutafakari kama hiyo ndiyo taswira wanayotaka kuiacha katika
jamii ya Watanzania,” amesema.
Amesisitiza kuwa vyombo vya habari
vina nafasi kubwa ya kuunda mtazamo wa jamii, hivyo kuna wajibu wa
kuhakikisha maudhui yanayotolewa yanajenga uelewa, yanakuza maendeleo na
yanalinda maslahi ya taifa.
“Tunachosimamia ni kuhakikisha
Mwandishi wa Habari anayepata ithibati anakuwa na kiwango cha elimu
kisichopungua Diploma, lakini tunataka pia Waandishi wa Habari waendelee
kupata mafunzo ili waweze kuimarika zaidi kitaaluma,” amesema.
Amesema
ipo haja ya sekta ya habari kutafakari aina ya maudhui yanayopewa
kipaumbele, akisisitiza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika
kujenga fikra na mwelekeo wa jamii.
0 comments:
Post a Comment