TBPL YATAKIWA KUHAKIKISHA UBORA WA MBOLEA HAI

Na Mwandishi Wetu, Kibaha

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameitaka Tanzania Biotech Production Ltd (TBPL) kuhakikisha inazingatia ubora katika uzalishaji wa mbolea hai ili kukidhi mahitaji ya soko na kulinda afya za watumiaji.

Kapinga alitoa kauli hiyo mjini Kibaha wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya ushirikiano kati ya TBPL, kampuni tanzu ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), na taasisi mbalimbali ikiwemo TFC, TARI, TFRA na TPHPA.

Alisema mbolea hai ina fursa kubwa sokoni kutokana na kutokuwa na kemikali hatarishi na uwezo wake wa kuhifadhi mazingira, jambo linaloifanya kuwa salama kwa afya ya binadamu na mazingira kwa ujumla.

“Mbolea hii ina soko kubwa na mchango wake katika kulinda mazingira ni muhimu. Hivyo, ni lazima ubora wake uzingatiwe wakati wote ili kuendelea kujenga imani kwa watumiaji,” alisema Kapinga.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mwendeshaji wa NDC, Nicolaus Shombe, alisema uzalishaji wa mbolea hai unaotarajiwa kufanywa na kiwanda hicho utachochea mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kuongeza tija na kuhamasisha matumizi ya pembejeo rafiki kwa mazingira.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TBPL, Mhandisi Rafael Moya, alisema mbolea hiyo itasaidia kupunguza matumizi ya kemikali katika shughuli za kilimo, huku ikichangia kulinda afya za wananchi na mazingira.

Alisema kipaumbele cha taifa kwa sasa ni kuhakikisha uzalishaji wa chakula unafanyika kwa njia salama na endelevu, huku wakulima wakinufaika na teknolojia na pembejeo zinazolinda afya na mazingira.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment