Na Mwandishi Wetu
Waandishi
wa Habari watakaoshiriki Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za
Maendeleo (Samia Kalamu Awards - SKA) 2026 wamelazimika kukidhi sharti
la kuwa na ithibati kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari
(JAB), hatua inayolenga kuimarisha weledi, uwajibikaji na ushindani wa
haki katika taaluma hiyo.
Akizindua
rasmi mchakato wa kupokea kazi za kushindanishwa, Jumapili Tarehe 31
Mei, 2026, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa SKA, Mha. Peter
Mwasalyanda, amesema maandalizi ya mwaka huu yanazingatia maelekezo ya
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kutambua mchango wa Waandishi
wa Habari za maendeleo nchini.
Mwasalyanda
amesema ili kuhakikisha uadilifu, uwazi na ushindani wa haki,
maandalizi ya tuzo hizo yanahusisha pia Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa
Habari (JAB) kama mdau muhimu katika kusimamia weledi na maadili ya
taaluma ya uandishi wa habari.
“Tuzo
hizi zinalenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui
ya ndani yenye ubora, yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na
kuburudisha, na kuimarisha taswira chanya ya Taifa kupitia habari za
maendeleo,” amesema.

Kwa
upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula,
amesema tofauti na msimu wa kwanza wa tuzo hizo, mwaka huu washiriki
wanapaswa kuhakikisha wamekidhi sharti la ithibati.
“Mtakumbuka
Msimu wa kwanza wa Samia Kalamu mambo ya JAB hayakuwepo, kwa hiyo
waandishi walishiriki wote bila kujali vigezo vya Ithibati lakini mwaka
huu kuna hiki kigezo cha kuwa na ithibati kwa hiyo niwashauri basi wote
wanaoshiriki kwenye hizi tuzo wahakikishe wanakuwa na ithibati,
wamethibitishwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari.” Amesema
Wakili Kipangula na kuongeza;

“Ni
muhimu sana kwa sababu ni takwa la kisheria na kitu ambacho hatuwezi
kukikwepa. Nawahamasisha tushiriki wote kwa sababu isionekane ni tuzo za
watu fulani tu, kila mmoja awasilishe kazi zake,” amesema Kipangula.
Kwa
mujibu wa vigezo vya ushiriki vilivyotangazwa, Waandishi wa Habari wa
Tanzania Bara wanatakiwa kuwa wamethibitishwa na JAB, huku kwa Zanzibar
washiriki wakitakiwa kuwa na kitambulisho cha Mwandishi wa Habari (Press
Card).
Tuzo hizo zimeanza kupokea kazi kuanzia Mei 31 hadi Juni 30, 2026 na zinatarajiwa kutolewa kati ya Oktoba na Desemba mwaka huu.








0 comments:
Post a Comment