
Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetumia Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Karibu-KiliFair 2026 kutangaza mafanikio ya mpango wa bima ya lazima kwa wasafiri, ikieleza kuwa umeimarisha usalama wa wageni na kuchangia ukuaji wa sekta ya afya pamoja na mapato ya utalii visiwani humo.
Mpango huo ulioanza kutekelezwa rasmi Oktoba 1, 2024, unawataka wageni wote wa kimataifa wanaoingia Zanzibar kuwa na bima ya usafiri kabla ya kuwasili. Tangu kuanzishwa kwake, mpango huo umeendelea kuwa chanzo muhimu cha mapato, ukiingiza wastani wa dola za Marekani milioni moja, sawa na zaidi ya Sh bilioni 2.6 kila mwezi.
Akizungumza na waandishi wa habari katika banda la Shirika la Bima Zanzibar (ZIC) kwenye viwanja vya Magereza jijini Arusha, Ofisa Mauzo wa shirika hilo, Abdul-Halim Muhammad, alisema maonesho hayo yamewapa fursa ya kutoa elimu kwa watalii, wawekezaji na wadau wa sekta ya utalii kuhusu umuhimu wa bima hiyo.
“Tunashiriki Karibu-KiliFair kuongeza uelewa kuhusu bima hii ya lazima na kueleza namna inavyowanufaisha wageni huku ikichangia maendeleo ya huduma muhimu Zanzibar,” alisema.
Kwa mujibu wa utaratibu huo, wageni wengi wa kimataifa hulipa dola 44 za Marekani kwa kila safari ya kuingia Zanzibar, huku wageni kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wakilipia dola 22 pekee. Watoto wenye umri wa miaka mitatu hadi 17 hulipa dola 22, huku walio chini ya umri huo wakisamehewa.
Muhammad alisema bima hiyo inawawezesha wageni kupata huduma za matibabu ya dharura na msaada mwingine muhimu wanapokuwa Zanzibar, hatua inayopunguza changamoto za kifedha na kuhakikisha wanapata huduma kwa haraka wanapozihitaji.
Alisema sehemu ya mapato yanayokusanywa kupitia mfuko huo hutumika kugharamia huduma za afya kwa wageni waliokatiwa bima, huku fedha zinazobaki zikielekezwa katika kuimarisha huduma za afya kwa wananchi na wageni kwa ujumla.
“Mpango huu ulianzishwa baada ya mamlaka kubaini kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya watalii na wawekezaji kuhitaji matibabu ya dharura huku kukiwa na sintofahamu kuhusu nani angegharamia huduma hizo. Sasa mfumo huu umeondoa changamoto hiyo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa KiliFair Promotions, Dominic Shoo, alisema Karibu-KiliFair 2026 imeendelea kuthibitisha nafasi yake kama maonesho makubwa ya utalii na biashara Afrika Mashariki kwa kuwakutanisha wadau kutoka zaidi ya nchi 40 duniani.
Alisema maonesho hayo yamevutia zaidi ya waoneshaji 500 na wanunuzi wa huduma za utalii wapatao 20,000, hatua inayochochea uwekezaji, ushirikiano wa kibiashara na upanuzi wa masoko ya utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Karibu-KiliFair ni jukwaa muhimu la kuitangaza Tanzania na Afrika Mashariki kimataifa. Kadri wadau wanavyoongezeka kushiriki, ndivyo fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa sekta ya utalii zinavyozidi kuongezeka,” alisema Shoo.
0 comments:
Post a Comment