TANZANIA, ALGERIA KUSHIRIKIANA KUKUZA UZALISHAJI WA DAWA NA VIFAA TIBA

Na Mwandishi Wetu.

ALGIERS: Tanzania na Algeria zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo na kukidhi mahitaji ya soko la ndani na la Afrika.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Viwanda vya Dawa wa Algeria, Dkt. Wassim Kouidri, katika ofisi za wizara hiyo jijini Algiers.

Katika mazungumzo hayo, Balozi Matinyi alimweleza Waziri Kouidri kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kuendeleza sekta ya viwanda vya dawa, ikiwemo kuweka vivutio maalum kwa wawekezaji.

Alisema tayari viwanda vitano vya dawa vinaendelea kujengwa nchini, huku vingine vikitazamiwa kuanzishwa katika kipindi kijacho.

“Serikali imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha viwanda vya dawa na vifaa vya tiba katika ukanda wa nchi za mashariki, kati na kusini mwa Afrika wenye watu takriban milioni 350,” alisema Balozi Matinyi.

Kwa upande wake, Waziri Kouidri aliahidi ushirikiano wa Serikali ya Algeria katika kuisaidia Tanzania kupata utaalamu wa kisasa wa utengenezaji wa dawa na vifaa tiba.

“Ni kweli, Tanzania ipo kwenye eneo zuri la kimkakati la ukanda mkubwa wa Afrika na Algeria iko tayari kushirikiana nayo kitaalamu ili kuhakikisha inafikia malengo yake,” alisema.

Aidha, Balozi Matinyi alikaribisha ziara ya Mamlaka ya Taifa ya Bidhaa za Dawa ya Algeria (ANPP), inayotarajiwa nchini Tanzania mwezi Oktoba mwaka huu kwa mwaliko wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA).

Ziara hiyo inalenga kujadili namna bora ya kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu kati ya mamlaka hizo katika sekta ya dawa.

Tanzania pia imeendelea kujijengea heshima barani Afrika katika udhibiti wa dawa baada ya kuwa nchi ya kwanza barani humo kufikia kiwango cha daraja la tatu la ukaguzi wa dawa (ML3) mwaka 2018, chini ya tathmini ya viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kiwango hicho hupima ubora na ufanisi wa mifumo ya udhibiti na ukaguzi wa dawa katika nchi.

Tangu mwaka 2020, nchi nyingine tisa za Afrika zimefikia kiwango cha ML3. Nchi hizo ni Afrika Kusini, Ethiopia, Ghana, Misri, Msumbiji, Nigeria, Rwanda, Senegal na Zimbabwe.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna nchi ya Afrika iliyofikia kiwango cha juu zaidi cha ML4.

Kwa upande wa Algeria, nchi hiyo ni miongoni mwa vinara wa sekta ya viwanda vya dawa na vifaa tiba barani Afrika ikiwa na viwanda 230, sawa na takriban theluthi moja ya viwanda 690 vilivyopo barani humo.

Ushirikiano huo unatarajiwa kusaidia Tanzania kuongeza uwezo wa uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kuongeza nafasi ya nchi katika soko la dawa la Afrika.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment