



---
Kilimanjaro-Moshi, Aprili 26,2015: Wasichana wanaosoma katika shule ya sekondari ya Weruweru iliyopo mkoani Kilimanjaro wametakiwa kufuata nyayo,kujifunza na kupata ushauri kutoka kwa wanawake wenye mafanikio katika jamii ambao utawaongoza kwa maisha yao ya baadaye baada ya kuhitimu masomo ya sekondari.
Ushauri huo umetolewa na Mtendaji Mkuu wa Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Georgia Mutagahywa katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa mahafali wa kidato cha sita ya shule hiyo yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyohudhuriwa na wazazi,walimu na wageni kutoka sehemu mbalimbali wakiwemo wanafunzi waliosoma shule hiyo miaka ya nyuma.
Katika mwendelezo wake wa jitihada za kuwawezesha watoto wa kike kwenye mahafali hayo, taasisi ya Vodacom Foundation imetoa msaada wa mashine ya kudurufu (Photocopy) kwa niaba ya wafanyakazi wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania itakayorahishisha kudurufu kazi za wanafunzi na walimu na kufanya mawasiliano na nukshi.
Vodacom imeona kuwa mashine hii ni moja ya hitaji kubwa kwa wanafunzi wa shule hiyo kwa kuwa itawapunguzia adha ya kupoteza muda mwingi kwenda kufuata huduma hizo kwa umbali mrefu ambapo muda huo wangeutumia kwa masomo yao na shughuli nyingine za kitaaluma na kwa mwaka huu imepatiwa heshima na uongozi wa shule hiyo kutoa mgeni rasmi katika mahafali hayo ya kidato cha sita.
Mkuu wa shule ya Weruweru Bi.Rosalia Tarimo ameishukuru taasisi ya Vodacom Foundation kwa msaada huo . “Tunatoa shukrani zetu za dhati kwa taasisi ya Vodacom Foundation kwa msaada huu wa mashine ya kisasa,huu ni uthibitisho kuwa Vodacom Foundation ni kinara katika mapambano ya kuwawezesha na kuwakomboa watoto wa kike na tunaomba taasisi nyingine zishiriki katika kampeni ya kuwawezesha watoto wa kike”Alisema.
Safari ya kuwakomboa watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali lakini jitihada za kuwakomboa zikifanyika kwa nguvu zote mafanikio yatapatikana hususani kuwafanya watoto wa kike wapate elimu bora waweze kujiamini na moja ya njia ya kufikia mafanikio ni kufuata nyayo,kujifunza na kupata ushauri kutoka kwa wanawake waliofanikiwa kwenye jamii mbalimbali.
Akiongea muda mfupi baada ya kukabidhi msaada huo,Mtendaji Mkuu wa Mawasiliano wa Vodacom Tanzania,Bi.Georgia Mutagahywa alisema Vodacom itaendelea kusaidia shule hiyo kukabiliana na changamoto mbalimbali mojawapo ikiwa kupitia wanafunzi waliosoma shuleni hapo. Shule hiyo pia inakabiliwa na matatizo ya kutokuwa na mtandao wa internet ambapo Vodacom imeahidi kulivalia njuga tatizo hilo kuhakikisha linamalizika.
“Tumetoa msaada huu kwa shule ya Weruweru na tumekuwa tukitoa misaada ya aina hii kwa taasisi mbalimbali kwa kuwa tunaamini kuwa kumkomboa mwanamke ni kukomboa jamii nzima na tunaamini kuwa wanawake wakiwezeshwa na kupata elimu bora wanaweze kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii yoyote ile”.Alisema
0 comments:
Post a Comment