MARIE STOPES TANZANIA KUADHIMISHA MIAKA 40 KWA KUTOA HUDUMA ZA AFYA BURE

Mkurugenzi Mkazi wa Marie Stopes, Anil Tambay (katikati) akiongea na waandishi wa habari kuelezea juu ya maadhimisho ya miaka 40 kwa kutoa huduma bure za uzazi wa mpango na uchunguzi wa kansa ya mlango wa kizazi kama maadhimisho ya miaka 40 ya Marie Stopes International. Maadhimisho hayo yanatarajia kufanyika Novemba 2-4, 2016 kwenye kliniki na hospitali zake zote nchini Tanzania.
Marie Stopes Tanzania itatoa huduma za uzazi wa mpango na uchunguzi wa kansa ya mlango wa kizazi bure kuanzia tarehe 2 hadi 4 Novemba kwenye kliniki na hospitali zake zote nchini kama sehemu ya kuadhimisha miaka 40 ya Marie Stopes International, na hivyo kuongeza idadi ya akina mama ambao wamewezeshwa kuwa na maamuzi juu ya mustakabali wa maisha yao wa kupata watoto kwa utashi na si kwa kubahatisha.

Marie Stopes Tanzania ni sehemu ya Marie Stopes International, shirika la kimataifa linalojihusisha na kutoa huduma za afya ya uzazi na lilianzishwa mwaka 1976. Katika wiki inayoanzia Oktoba 31, tutakuwa tuaadhimisha miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Maries Stopes International.

Kwa miaka 40 tangu kuanzishwa kwake, Marie Stopes International imepanuka kutoka kuwa na zahanati moja jijini London, na kuwa shirika la kimataifa linalotoa huduma bora na nafuu za uzazi wa mpango katika nchi 37 duniani. Mwaka jana wanawake milioni 21 duniani walikuwa wanatumia angalau njia moja wapo ya uzazi wa mpango kwa kuhudumiwa na Marie Stopes International, ikiwa ni sehemu ya watumiaji wa uzazi wa mpango wapatao milioni 291. Marie Stopes International inanuwia kuzidisha takwimu za matokeo ya kiafya kwa kutoa huduma za uzazi wa mpango kwa watumiaji wapya wapatao milioni 12 ifikapo kwaka 2020. Hii ni sawa na asilimia 10 ya ahadi ya Mpango wa Kimataifa kwa mwaka 2020 wa Uzazi wa Mpango, yaani FP2020, inayolenga kuwafikia watumiaji wapya milioni 120 wa huduma za uzazi wa mpango ifikapo mwaka 2020. Tangu kujiwekea ahadi hii, tayari mamilioni ya mimba zisizotarajiwa zimeweza kuepukika, na maelfu ya vifo vinavyotokana na uzazi kwa akina mama vimepungua. Tumenuia kuchukua muelekeo huu, kufanya kazi zaidi na hata kuchukua hatua stahiki zaidi.

Kwa hapa nchini, shirika la Marie Stopes ilianzishwa mwaka 1989 na limeendelea kuwajibika kulingana na dhamira ya shirika. Mwaka jana, wanawake 447, 617 nchini walinufaika na huduma za uzazi wa mpango na hivyo kuwapa uwezo wa kuchagua lini na ama kusubiri kupata mtoto.

“Tumedhamiria kuendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika kutimiza mpango wa kitaifa wa kuongeza matumizi ya njia za uzazi wa mpango kutoka asiliamia 32 kwa mwaka 2015 mpaka asilimia 45 kwa mwaka 2020, hasa kwa akina mama na wasichana. Hii ni sawa na ongezeko la watumiaji wapya wa uzazi wa mpango kutoka milioni 2.6 kwa mwaka 2016 hadi kufikia milioni 4.2. Marie Stopes Tanzania inalenga kuwafikia watumiaji wa njia za uzazi wa mpango milioni mbili hadi ifikapo mwaka 2020, kama njia ya kuendeleza jitihada za Serikali,” amesema Bw.Anil Tambay, Mkurugenzi Mkazi wa Marie Stopes.

Tunapoadhimisha miaka 40 ya Marie Stopes International, Marie Stopes Tanzania inaahidi kuboresha jitihada zake na kujikita katika maeneo yafuatayo, kati ya sasa na mwaka 2020 hapa nchini:

· Kuzifikia jamii za maeneo ya vijijini kwa huduma za uzazi wa mpango, hasa kwa akina mama na vijana. Tunaahidi kuhakikisha kuwa asilia 70 ya watakaofikiwa kwa kutumia njia za uzazi wa mpango ni wale watu masikini wanaoishi chini ya Dola Moja wa Kimarekani kwa siku (sawa na Sh. 2,730) na takriban asilimia 20 vijana chini ya miaka 20. Tayari tunaendesha huduma za mkoba (outreach teams) 35 katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar.

· Tunafanya kazi na mamlaka za Serikali Kuu, Mikoani na ngazi za Wilaya ili kuboresha ubora wa huduma. Zaidi ya watoa huduma wa Serikalini 600 wameweza kupata mafunzo kutoka kwetu kwa mwaka jana na kwa sasa wanaendelea kutoa huduma. Watumishi Zaidi watapewa mafunzo kama sehemu ya kujengea uwezo sekta ya umma.

· Kufanya kazi na Taasisi zisizokuwa za kiserikali (NGOs) kujenga hoja na ushawishi katika kuboresha bajeti na sera husika. Mpango Mkakati wa kuboresha Afya ya Uzazi, watoto na Vijana waliofikia umri wa kubarehe ya mwaka 2016-2020 inaonyesha kuwa karibu Dola milioni 75 zinahitajika kununua na kusambaza dawa na vifaa tiba vya uzazi wa mpango kwa kila mwaka, lakini bado kitaifa tuko nyuma sana kufikia lengo hilo. Tutashawishi kuwepo kwa jitihada hahsusi kutenga rasilimali kwa ajili ya kupambana na mimba za utotoni na zile zisizotarajiwa miongoni mwa vijana, takwimu ambayo inaongezeka badala ya kupungua (takriban asilimia 27 ya wasichana wadogo walianza kuzaa watoto katika mwaka 2015 ikilinganishwa na asilimia 23 kwa mwaka 2010).

Nchini Tanzania, Marie Stopes itasherekea maadhimisho ya miaka 40 kwa kutoa huduma bure kwa wateja wetu kama namna ya kuwashukuru kwa imani yao toka kuanzishwa kwetu hadi sasa. Bw. Tambay alisema, “tunajivunia nafasi tuliyonayo katika kuitekeleza dhamira ya Marie Stopes International ya Wototo kwa Utashi na si kwa Kubahatisha. Shirika hili liliundwa ili kuwawezesha wanawake na familia kupata haki yao ya kuchagua kama wanataka kuwa na watoto na lini wapate watoto, hivyo Marie Stopes Tanzania imedhamiria kuhakikisha watanzania wanaipata haki hiyo.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment