Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku moja wa Tume na asasi za kiraia kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano huo umefanyika leo Julai 30, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa siku moja wa Tume na asasi za kiraia kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano huo umefanyika leo Julai 30, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki kutoka asasi za kiraia wakifuatilia mada katika mkutano huo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg. Kailima Ramadhani akizungumza wakati wa Mkutano wa siku moja wa Tume na asasi za kiraia kuhusu uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mkutano huo umefanyika leo Julai 30, 2025 Jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa onyo na maelekezo kwa taasisi na asasi za kiraia 164 zilizopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura kuhakikisha zinafuata sheria, kanuni, na maelekezo ya Tume wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Wito huo umetolewa leo, Julai 30, 2025 na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano maalum kati ya Tume na wawakilishi wa taasisi na asasi hizo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
“Nitoe rai kwenu mnaotekeleza jukumu hili la kutoa elimu ya mpiga kura: zingatieni sheria, kanuni, na maelekezo ya Tume wakati wote wa utekelezaji. Hili ni jukumu nyeti kwa mustakabali wa taifa letu,” alisisitiza Jaji Mwambegele.
Kwa mujibu wa Jaji Mwambegele, Tume imejipanga kushirikiana kwa karibu na mashirika yote yaliyopata vibali, ili kuhakikisha elimu hiyo inawafikia walengwa kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa asasi hizo kuwahimiza wananchi kuzingatia sheria na kudumisha amani kipindi chote cha kampeni.
Ameeleza kuwa historia ya chaguzi nchini inaonyesha uwepo wa joto la kisiasa wakati wa kampeni, na hivyo kuwataka wadau hao kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa uvumilivu na kuepuka vitendo vya uchochezi.
Kwa mujibu wa Kifungu cha 10(1)(g), (h) na (i) cha Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya Mwaka 2024, Tume ina wajibu wa kutoa, kuratibu, na kusimamia elimu ya mpiga kura nchini na pia kuratibu waangalizi wa uchaguzi.
Katika uchaguzi wa mwaka huu, jumla ya taasisi 164 zimepata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura, wakati taasisi 76 za ndani na 12 za kimataifa zimepata vibali vya kuwa waangalizi wa uchaguzi.
Wawakilishi wa baadhi ya asasi hizo, akiwemo Mwalimu Neema Kabale kutoka Malezi Foundation Network, wameeleza kuwa wamejipanga vizuri kuwafikia vijana – hususan wale wanaopiga kura kwa mara ya kwanza – ili kuwapa uelewa sahihi wa haki na taratibu za uchaguzi.
“Tunaamini elimu sahihi kwa mpiga kura, hasa kwa vijana, ni msingi wa uchaguzi huru, haki na wenye amani,” alisema Mwalimu Kabale.
Washiriki kutoka asasi za kiraia mbalimbali wakichangia hoja wakati wa majadiliano.
0 comments:
Post a Comment