Serikali yawataka Vijana kuzingatia vigezo ili wapate mkopo

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Vijana Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo anayesimamia Kitengo cha Uratibu na Uwezeshaji Dr. Steveni Kissui (aliyesimama) akifungua mafunzo ya jinsi ya kujikwamua na umasikini kwa Vijana wa Manispaa ya Singida,Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Ester Riwa.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Ester Riwa aliyesimama akivifundisha vikundi mbalimbali vya vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida mjini namna ya kuandika miradi ya maendeleo,mafunzo hayo yamefanyika Wilayani humo ikiwa ni juhudi za Serikali kuwakwamua vijana katika matatizo yanayowakabili.
Afisa Vijana wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutoka Idara ya Maendeleo ya Vijana Bi. Amina Sanga akitoa mada ya jinsi ya Mfuko wa Vijana unavyofanya kazi.

Afisa Vijana wa Mkoa wa Mbeya Bw. Masele Lauriani Akitoa mada ya jinsi ya kuwa mjasiriamali katika mafunzo yanayoendeshwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa Vijana wa Mkoa wa Singida.

Benjamin Sawe, WVUM, Singida

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imewaasa vijana wa kikundi cha Mapambano Vijana Saccoss kuzingatia vigezo wanapoomba mikopo katika mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Hayo yalisemwa jana na Mkurugenzi  Msaidizi Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo anayesimamia Kitengo cha Uratibu na Uwezeshaji Dr. Steveni Kissui alipotembelea  Ofisi  ya Mapambno Vijana Saccoss Ltd iliyopo Manispaa ya Singida mjini.

“Vikundi vya vijana wanaoomba mkopo katika Mfuko wa Vijana ni vyema wakazingata vigezo vinavyotakiwa kufuatiliwa pale wanapoomba mikopo kwani muongozo upo wazi na unaelekeza vizuri hivyo kwa kufanya hivyo suala la kupata mkopo kwa wakati kupitia mfuko huo utakuwa rahisi, kwa mfano kigezo cha umri ni muhimu kuzingatiwa ikibainisha umri wa kijana ni kuanzia miaka 15 hadi 35” Alisema Bw. Kissui.

Naye Mwenyekiti wa Mapambano Vijana Saccos Bi. Halima Sadiki amewashauri vijana wenzake kuacha kulalamika badala yake wajiunge na kuanzisha vikundi ili kuweza kupata mkopo na kuweza kujitatulia matatizo yao.

“Tunaushukuru sana uongozi wa Wizara ya Habari,Vijana Utamaduni na Michezo, kwa kutuma viongozi wake kututembelea hapa Manispaa ya Singida na kutupatia elimu juu ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ikiwemo mambo ya kuzingatia tunapounda vikundi vya vijana”,alisema Bi Halima.

Hata hivyo serikali imewashauri vijana hao kuandika mradi na kuainisha mchanganuo wake vizuri pale watakapo omba mkopo na kuzingatia mambo yote muhimu yaliyopo katika mwongozo kwani serikali imedhamiria kuwakomboa vijana kwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.

Wakati huohuo Dr. Kissui alisema kumekuwa na dhana miongoni mwa Vijana kuwa Serikali ndio mwajiri Mkuu na kusahau kuwa ujasiriamali ndio suluhisho pekee la tatizo la ajira kwa Vijana.

“Vijana mnatakiwa kujiunga ikiwa ni pamoja na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za ujasiriamali na kuacha tabia ya kulalamika, Alisema Dr. Kissui.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment