BODI YA MANUNUZI NA UGAVI (PSPTB) YATOA MAFUNZO KWA WANAFUNZI WA CHUO CHA UHASIBU MBEYA

 Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Winfrida Igogo akitoa mada katika mafunzo ya wanafunzi wanaosoma masomo ya manunuzi na ugavi katika Chuo cha TIA Mbeya.
Wanafunzi ambao wanasoma masomo ya manunuzi na ugavi wakifuatilia mafunzo yaliyotolewa na Bodi ya manunuzi na ugavi katika chuo cha uhasibu Mbeya.
 --- 
Na Mwandishi Wetu 

BODI ya manunuzi na ugavi (PSPTB) imetoa mafunzo kwa wanafunzi waosoma masomo ya manunuzi na ugavi katika chuo cha uhasibu(TIA) Mbeya. Katika mafunzo hayo wito ulitolewa kwa Taasisi binafsi na serikali kuepuka kutoa ajira katika sekta ya manunuzi na ugavi kwa watu ambao hawana taaluma hiyo wala kusajiliwa na Bodi ya PSPTB. 

Wito huo ulitolewa na Mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Manunuzi na ugavi(PSPTB), Winfrida Igogo, alipokuwa akijibu maswali kutoka kwa Wanafunzi wa taasisi ya Uhasibu kampasi ya Mbeya ambao ni wanachama wa Umoja wa wanataaluma wa manunuzi na Ugavi(PSA-TIA) wakati wa mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa TIA Mbeya. 

Igogo alisema hairuhusiwi kwa mtu yoyote kufanya kazi za manunuzi na ugavi bila kuwa na utalaam pamoja na kusajiriwa na bodi kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria jambo ambalo adhabu inamkumba pia mwajiri. Alisema lengo la kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya manunuzi na ugavi(procurement & supply)ni kuwajengea uwezo na kuwahamasisha juu ya taratibu wanazopaswa kuzifuata wakiwa kazini kuhusiana na manunuzi na ugavi. 

Aliongeza kuwa lengo lingine ni kuwakumbusha wanataaluma hao kujisajili na bodi mara baada ya kuhitimu masomo yao jambo ambalo litasaidia upatikanaji wa ajira haraka tofauti na wasio sajiliwa ambao hukaa muda mrefu bila ajira kutokana na kukosa kipengere cha uzoefu. 

Alisema Bodi ipo kwa mujibu wa sheria ambapo hivi sasa ipo kwenye mchakato wa kupitia kila taasisi kukagua kama walioajiriwa wanasifa za manunuzi na ugavi ikiwa pia kupitia matangazo mbali mbali ya ajira kama vigezo vinavyowekwa vipo kwa mujibu wa sheria. Kwa upande wake Mwezeshaji mwingine katika mafunzo hayo, Juvenal Joseph, alisema ni vema wataalamu wa manunuzi na ugavi wakazingatia sheria kwa kuepuka mikataba inayoweza kuwaingiza matatizoni. 

Alisema wataalam wa manunuzi na ugavi wanapaswa kujua kuwa kila mikataba ni makubaliano lakini sio kila makubaliano yanaweza kuwa mikataba hivyo wajiepushe kutumbukia katika rushwa kwa kukiuka taratibu za manunuzi na ugavi. 

Naye Mlezi wa Wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu (TIA) Kampasi ya Mbeya aliyejitambulisha kwa jina moja la Mgaya alisema Wanafunzi wanaosomea masomo ya manunuzi na ugavi wanapaswa kuwa na nidhamu katika masomo yao ili kuepuka kuwa maafisa wav yeti. 

Aidha Mwalimu wa Somo la Manunuzi na ugavi chuoni hapo, aliyejitambulisha kwa jina la Gasibila aliishukuru bodi kwa kuendesha mafunzo hayo na kuongeza kuwa jambo hilo litasaidia kuzalisha wahitimu wenye taaluma na kupata watumishi waliotukuka. 

Aliongeza kuwa waalimu na watumishi katika fani ya manunuzi na ugavi wanategemea maelekezo kutoka miongozo kutoka bodi kwa kuwa wao ndiyo dira ya utumishi mzuri nchini.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment