Mdau wa maendeleo, Jackson Kiswaga (mwenye skafu) akiwakabidhi moja ya mabati 50 wanafunzi wa shule ya sekondari ya Ufundi ya Ifunda kwa ajili ya ukarabati wa jengo la taaluma na nidhamu lilounguamwaka 2013 katika shule hiyo.(picha na Denis Mlowe)
Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini Jackson Kiswaga akivishwa skafu na moja ya skauti wa shule ya sekondari ya Ufundi ya Ifunda
Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini Jackson Kiswaga akikagua gwaride wa skauti wa shule ya shule ya sekondari ya Ufundi ya Ifunda
Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini Jackson Kiswaga akizungumza wanafunzi na wazazi wa shule ya shule ya sekondari ya Ufundi ya Ifunda
Mkurugenzi wa Tigo Nyanda za Juu Kusini Jackson Kiswaga akikabidhi cheti kwa mhitimu wa shule ya shule ya sekondari ya Ufundi ya Ifunda kidato cha sita.(picha na Denis Mlowe)
---
NA DENIS MLOWE, IFUNDA
WAZAZI wa wanafunzi wanaosoma shule ya sekondari ya Ufundi ya Ifunda iliyoko wilaya ya Iringa wamechangia mifuko ya saruji na misumari kwa ajili ya kuunga mkono ukarabati wa jengo la taaluma na nidhamu liloungua katika shule hiyo mchango wenye thamani ya shilingi 600,000.
Michango hiyo ambayo ilijumuisha fedha taslimu kwa lengo la kununua saruji na misumari ilitokana na juhudi za mgeni rasmi Jackson Kiswaga wa mahafari ya 14 ya shule hiyo ya kidato cha sita kuhamasisha ujenzi wa jengo hilo baada ya taarifa kutoka kwa mkuu wa shule Madi Kissuu aliyotoa kwa wazazi na kukabiliwa na changamoto ya ujenzi baada ya kuungua kwa moto.
Akizungumza katika mahafari hayo, Kiswaga ambaye alichangia mabati 50 papo hapo ili zisaidie katika ukarabati wa jengo hilo lililoungua moto mwaka 2013 alisema kuwa jukumu la uchangiaji wa sekta ya elimu sio kuachiwa serikali bali la kila mzazi anayependa maendeleo ya elimu katika nchi ya Tanzania.
Alisema wanafunzi ni lazima wasome kwa bidii ili watengeneze maisha yao ya baadaye kwani elimu ndio urithi pekee usiofananishwa na mali zingine za dunia kwani ni wa kudumu katika maisha yote ya binadamu hivyo juhudi ya mzazi kumuunga mkono mtoto katika kupata elimu iliyo bora na katika mazingira rafiki kwa mwanafunzi.
Kiswaga aliwataka wanafunzi hao kuacha tabia hatarishi zikiwemo utoro, uzinzi, ulevi na kila aina ya mambo yanayorudisha nyuma uelewa wao katika masomo shuleni hapo.
“Hakuna mtu mjinga dunia kama sio kichaa au una tatizo la ubongo. Kumbukeni kuwa MUNGU aliweka masaa 24 na kila mmoja akitumia saa 24 kwa uhakika katika maisha yake lazima kuna mambo ambayo atafanya kuweza kujiletea maendeleo yake na wanafunzi pia mna masaa hayo hayo ni wakati wako sasa kuamua unataka kuwa nani kesho na njia pekee ni kushikilia masomo na hapo ndipo ukichagua yaliyo mazuri unaweza kubadilisha maisha yako na ya jamii inayomzunguka,” alisema.
Alisema Tanzania inahitaji wasomi ili ijiletee maendeleo na kushindana kiuchumi na nchi nyingine hivyo ni muhimu wanafunzi wakaendelea kuhimili vikwazo wakati wakitafuta elimu zao.
Kwa upande wake Mchungaji Kedi Patrick kutoka nchini Uganda aliyeambatana na mgeni rasmi Jackson Kiswaga, aliwataka wazazi na wanafunzi kutambua kuwa elimu ndio chanzo kikubwa cha mabadiliko katika taifa lolote hapa duniani.
Alisema kuwa urithi pekee kwa watoto ni elimu na kusisitiza kuwa unaweza kumwachia mali, lakini itakwisha, ukimwachia elimu hakika huu ndiyo urithi pekee.
Naye mkuu wa shule hiyo, Madi Kissu alisema kuwa shule hiyo inakabiliwa na changomoto nyingi zinazohitaji juhudi za pamoja kuzitatua hasa katika uchakavu wa majengo na kukosekanika kwa walimu wa masomo ya sayansi.
Katika mahafari hayo ya 14 jumla ya wanafunzi 324 wanatarajia kumaliza elimu ya kidato cha sita yaliambatana na gwaride la heshima lilotolewa na skauti wa shule hiyo sambamba na kukabidhiwa vyeti kwa wanafunzi wote na zawadi kwa walimu waliofanya vizuri katika kufaulisha masomo yao.
0 comments:
Post a Comment