MAABARA YA MAFUNZO ITEMBEAYO YAZINDULIWA RASMI

DSC_0080
Mganga Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth Mhando akisoma hotuba ya uzinduzi wa maabara itembeayo kwa ajili ya mafunzo ya upasuaji. Kulia ni Naibu Balozi wa Ireland nchini, Maire Matthews na kushoto ni Mkurugenzi wa ECSA anayeshughulikia Afya ya jamii Prof Yoswa Dambisya.

Na Mwandishi wetu
Mganga Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Magreth Mhando mwishoni mwa juma alizindua maabara ya upasuaji ya mafunzo inayotembea iliyotolewa kwa chuo kitembeacho cha COSECSA na serikali ya Ireland.

Alifanyakazi hivyo kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa jamii, Dk Seif Rashid.

Maabara hiyo ambayo ni mradi wa majaribio wa chuo hicho wenye lengo la kufundisha wapasuaji pale walipo imegharimu dola za Marekani 100,000.
Kwa mujibu wa taarifa za COSECSA maabara hiyo itakuwa nchini kwa miezi kama mitatu kabla ya kwenda Kenya na baadae Malawi.

Mradi huo wenye lengo la kufundisha wapasuaji zaidi kwa kufika eneo ambalo wanafanyia kazi, ni moja ya miradi ya chuo kitembeacho ambacho toka kimeanzishwa mwaka 1990 kimeshatoa wapasuaji 200.

Hafla ya uzinduzi wa maabara hiyo yenye vifaa vya kisasa vya kufundishia na kufanyia upasuaji ikiwamo ya upasuaji kwa kutumia darubini ulifanyika katika hospitali ya kumbukumbu ya Hubert Kairuki.
DSC_0053
Rais wa COSECSA , Profesa Stephen Ogendo akisoma taarifa kwa mgeni rasmi kabla ya uzinduzi.
Akizindua maabara hiyo Dk. Mhando alisema kwamba ni matumaini yake italeta mabadiliko makubwa katika kuwezesha taifa kuwa na wataalamu wengi wa upasuaji.
Aidha alisema changamoto ya kutosajiliwa kama chuo kamili wakati mataifa mengine yamefanya atayafuatilia ili kuweza kuona ya kukiwezesha chuo hicho kutambuliwa rasmi nchini Tanzania.

Maabara hiyo mali ya College of Surgeons of East Central and Southern Africa (COSECSA) iliwasili mapema mwezi huu na jana ndio ilikuwa uzinduzi rasmi ambao ulishuhudiwa na wanafunzi wa upasuaji, wataalamu na maofisa mbalimbali wa afya wakiwemo watu wa Mfuko wa taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Kaimu mkurugenzi wa Mfuko huo Michael Mhando alisema kwamba wamefurahishwa na juhudi za wadau wao katika kuimarisha vifaa tiba na utoaji wa wataalamu.
Alisema anaamini kwamba maabara hiyo ni moja ya mambo muhimu yanayotakiwa kufanywa na wadau ili kuimarisha tiba nchini.

Alisema kwamba wataangalia namna ya kufanya ili kusaidia huduma hiyo kwani inahitajika sana vijijini ambako wengi wa watu hawapati fursa ya kufanyiwa upasuaji hata ule mdogo.
DSC_0130
Baadhi ya wadau wa sekta ya afya na wanafunzi waliohudhuria hafla hiyo.
Maabara hiyo yenye uzito wa tani 30 inatarajia kufanya mafunzo ya upasuaji katika hospitali zenye uhusiano na COSECSA.

Aidha maabara hiyo inaweza kufunza wapasuaji 10 kwa mkupuo mmoja.
Kuletwa kwa maabara hiyo kutoka Ireland ambako kuna uzoefu wa miaka mingi wa kutumia maabara zitembeazo za upasuaji kumefanikishwa na mahusiano yaliyopo kati ya Royal College of Surgeons in Ireland (RCSI), Shirika la misaada la Ireland (Irish Aid) na College of Surgeons of East, Central and Southern Africa (COSECSA).

Maabara ya mafunzo ya upasuaji itembeayo ilianzishwa na RCSI kwa mara ya kwanza duniani mwaka 2006 na kwa uzinduzi uliofanyika dare s Salaam jana umedhihirisha dhamira njema ya COSECSA na RCSI ya kutoa mafunzo bora kwa lengo la kuimarisha afya za wanadamu.

Akizungumza kwenye tukio hilo Rais wa COSECSA , Profesa Stephen Ogendo alisema kwamba kuwepo kwa maabara hiyo kutasababisha mabadiliko makubwa katika utoaji mafunzo katika ukanda wa Afrika Mashariki, kati na Kusini ( ECSA).

Alisema kwamba kutokana na uasili wa maabara hiyo wanafunzi hawatakuwa wanalazimika kufuata kituo cha mafunzo na badala yake kituo hicho kitawafuata pale walipo.

Aidha alisema kwamba muundo na mfumo wa ufundishaji umeshatengenezwa kwa ajili ya kusaidia mafunzo hayo kwa nchi wanachama.
DSC_0023
Naye Mkurugenzi wa ECSA anayeshughulikia Afya ya jamii Prof Yoswa Dambisya alisema kwamba wataendelea kuwa mstari wa mbele kufundisha wataalamu wa afya kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisasa na zenye kutoa tija kama kuwepo kwa mabara hiyo.

Alisema kutokana na haja kubwa ya wataalamu wa upasuaji kuwepo kwa maabara hiyo itembeayo kutasaidia kufunza wanafunzi wengi katika eneo ambalo uwiano wa wataalamu na wagonjwa ni mtaalamu mmoja kwa wagonjwa 190,000 ukilinganisha na Uingereza ambako uwiano ni mtaalamu mmoja kwa wagonjwa 2,800.

Alisema raslimali kama ya maabara itasaidia kufunza watu wengi zaidi ili kuendelea kupunguza pengo la wataalamu wa upasuaji.

Alisema pia kwamba takwimu za dunia zinaonesha kuwa asilimia 6.5 ya magonjwa yanatokana na kukosekana kwa huduma za upasuaji.

Alisema vifo vingi vinatokana na kukosekana kwa huduma za upasuaji kuliko Malaria, Ukimwi na kifua kikuu kwa pamoja.

COSECSA ambayo ilianzishwa mwaka 1999 kwa malengo ya kutoa elimu ya upasuaji ilianzishwa na shirikisho la wapasuaji Afrika Mashariki ambalo lina miaka takaribani 60.
DSC_0087
Mganga Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth Mhando akikata utepe kuzindua maabara ya upasuaji ya mafunzo inayotembea iliyotolewa kwa chuo kitembeacho cha COSECSA na serikali ya Ireland.
DSC_0097
Mmoja wa walimu ambaye ni daktari bingwa wa upasuaji akitoa maelezo kwa mgeni rasmi Mganga Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth Mhando aliyemwakilisha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na Naibu Balozi wa Ireland nchini, Maire Matthews.
DSC_0146
Wageni mbalimbali wakiangalia namna maabara hiyo inavyofanyakazi.
IMG_2862
Mganga Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa jamiii, Dk. Magreth Mhando (kulia) akishuhudia zoezi la upasuaji kwa vitendo ndani ya maabara hiyo.
DSC_0151
Rais wa COSECSA , Profesa Stephen Ogendo akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kukagua maabara hiyo katika uzinduzi huo.
DSC_0090
Picha ya pamoja baada ya uzinduzi.
DSC_0047
Maabara ya upasuaji ya mafunzo inayotembea iliyotolewa kwa chuo kitembeacho cha COSECSA na serikali ya Ireland.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment