WADAU na wanaharakati wa maendeleo ya watoto leo wanaungana na jamii ya kimataifa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika kwa kuwahimiza wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kuingiza ajenda ya mtoto katika kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni 16 kila mwaka tangu mwaka 1991 kwa lengo la kuhamasisha jamii kujadili, kutathmini na kuweka mikakati ya kuboresha maisha ya mtoto wa kiafrika kama msingi wa kujenga taifa bora.
Siku ya mtoto wa Afrika ilianzishwa na Jumuiya ya Umoja wa Afrika (OAU) na kuadhimishwa kwa mara ya kwanza Juni 16, 1991 ili kuwahimiza viongozi kujenga utashi wa kisiasa wa kushughulikia matatizo yanayowakabili watoto wa Kiafrika kwa kuweka sheria za kuwalinda pamoja na kuwajengea mazingira bora ya kuishi.
Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika sanjari na maadhimisho ya miaka 25 ya Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto kwa kutumia kaulimbiu isemayo,” Tuunganishe juhudi zetu kutokomeza ndoa za utotoni Afrika.
Wanaharakati na wadau wa maendeleo na haki za watoto wametumia maadhimisho ya mwaka huu kujadili na kutathmini hotuba za wanasiasa waliojitokeza hivi karibuni kutangaza nia ya kugombea urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kubaini kuwa hakuna mgombea aliyeweka bayana jinsi atakavyotetea haki za watoto.
Wagombea zaidi ya 30 kutoka Chama Cha Mapinduzi ambao wamejitokeza na kuchukua fomu za kugombea nafasi kupeperusha bendera ya CCM katika kinyang’anyiro cha kugombea urais.
Baadhi ya wagombea ambao wameshajitokeza kuwania nafasi hiyo ni pamoja na Edward Lowassa, Bernard Membe, Profesa Mark Mwandosya, January Makamba, Lazaro Nyalandu, Mwigulu Nchemba, Mwele Malecela na Dk Hamis Kigwangalla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba anasema hali ya mtoto wa Tanzania inahitaji kuimarishwa kwa kuwa watoto wengi wamekumbwa na matukio mbalimbali ya kikatili lakini na sheria haijatekelezwa ipasavyo ili kuwalinda haki ya mtoto.
Bisimba anasema ingawa Tanzania inasheria za kuwalinda watoto, ukiukwaji wa sheria hizo ni mkubwa hali inayosababisha watoto kupata mateso ikiwa ni pamoja na watoto wenye ulemavu kufichwa ndani, wengine kukatwa mikono, kuunguzwa na moto, ndoa na mimba za utotoni, kulawitiwa, kubakwa na kutupwa.
Viongozi wanaotaka kuingia madarakani wanapaswa kuonesha utashi wa kisiasa katika kukomesha ukatili, kukataliwa au kupuuzwa, utumikishwaji na udhalilishaji dhidi ya watoto. Kwa mujibu wa ripoti ya Unicef ya mwaka 2014 watoto zaidi ya bilioni moja wenye umri kati ya mwaka mmoja hadi miaka 14 wanapata mateso kutokana na ukatili na adhabu zinazoambatana na shambulio la mwili.
Bisimba anasema katika kipindi hiki cha maandalizi ya uchaguzi mkuu wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi wanapaswa kuweka ajenda za mtoto katika kampeni zao ili kuwaenzi viongozi walioanzisha Siku ya Mtoto wa Afrika.
Endapo wanasiasa wanaogombea nafasi mbalimbali utashi wa kisiasa na kujumuisha ajenda ya watoto na kuelezea wakati wa kampeni za uchaguzi itasaidia kuhimia utekelezaji wa sheria za kulinda haki za watoto mara watakapoingia madarakani.
Bisimba anasema sheria za kulinda haki za watoto zinapaswa kuangaliwa vyema ili kuzuia watoto kufundishwa mambo yasiostahili kwa umri wao au mambo yasioendana na maadili ya Taifa.
Mfumo wa ulinzi wa watoto pamoja na matunzo ndio unaotoa picha na mwanga bora wa maendeleo ya mtoto kwa kizazi kijacho, huku wanasiasa wanapochaguliwa katika nyadhifa zao kuhakikisha wanasimamia yale wanayoyatolea ahadi kabla ya kuingia madarakani.
Kampeni za Uchaguzi Mkuu pamoja na kampeni za kura ya maoni kwa ajili ya Katiba pendekezwa zinapaswa kuzungumzia kwa uwazi juu ya utekelezwaji wa sheria na sera ya maendeleo ya mtoto ili kuweka msingi mzuri ya utekelezaji wa ajenda ya watoto. Ajenda ya Watoto ni mpango shirikishi unaojumuisha mashirika ya kimataifa, serikali, asasi za kiraia na wadau wengine waliojikita katika harakati za kutetea haki za watoto.
Lengo la ajenda ya watoto ni kuhamasisha wadau wa maendeleo kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa ili kujumuisha masuala ya watoto katika programu za maendeleo. Pia kuhamasisha wananchi ili kuishawishi serikali kuongeza bajeti katika vipaumbele vya mpango wa utekelezaji kwa ajili ya watoto, katika ngazi ya Serikali Kuu na serikali za mitaa kwa lengo la kufikia malengo ya kuboresha maendeleo ya watoto.
Wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani wanapaswa kuweka mkakati na kueleza dhamira ya dhati ya kumaliza kabisa umasikini wa watoto katika nyanja zote kwa kujumuisha program za maendeleo ya watoto katika mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini.
Pia wanasiasa wanatakiwa kueleza umma ni jinsi gani watapambana na ukatili dhidi ya watoto wa kike kwa kuweka sheria kali na kusimamia utekelezaji wa sheria ili kukomesha ndoa za utotoni, vipigo na udhalilishaji wa watoto wanaotumikishwa kwenye biashara ya ngono na watoto wa jinsia zote wananyimwa fursa ya kusoma na kutumishwa kazi mbalimbali.
Kwa mujibu wa ripoti ya haki za binadamu ya mwaka 2014 kuhusu ukatili na ndoa za utotoni, Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya ndoa za utotoni. Ripoti ya utafiti uliofanywa mwaka 2010 inaonesha kuwa asilimia 37 ya wanawake wa umri kati ya miaka 20 hadi 24 waliolewa wakiwa bado hawajafikisha umri wa miaka 18.
Mikoa ambayo inakabiliwa na tatizo la ndio za utotoni na asilimia ya kiwango chake katika mabano ni pamoja na Shinyanga (59), Tabora (58), Mara (55) Dodoma (51), Lindi (48), Mbeya (45), Morogoro (42), Singida (42), Rukwa (40), Ruvuma (39), Tanga (29), Arusha (27), Kilimanjaro (27), Kigoma (26), Dar es Salaam (19), na Iringa (8).
“Tunawashauri wagombea wa nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu ujao watumie takwimu hizi kuelezea ni jinsi gani watasaidia kuondoa tatizo la ndoa za utotoni,” anasema Bisimba. Watoto nchini Tanzania wameendelea kukumbana na matukio ya kikatili yanayofanywa na ndugu, wanafamilia na jamaa wa karibu ambao kimsingi wanapaswa kuwalinda.
Kwa kutazama matukio mbalimbali ya kikatili ambayo watoto hukumbana nayo, ipo haja kwa wagombea wanaotangaza nia ya kugombea uongozi kuweka dhamira ya dhati ya kuendelea haki na misingi bora kwa maendeleo ya watoto ili kuwandaa kuwa vijana bora wenye uwezo wa kuendelea nchi kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Vipaumbele vya wanasiasa vioneshe jinsi gani wanavyoweza kusimamia masuala ya watoto kwa kutambua kuwa nusu ya Watanzania ni watoto ambao wanahitaji kuwekewa sheria za kuwalinda na sera bora ili kujenga Taifa lenye nguvu kwa kutumia rasilimali watu iliyoandaliwa vizuri.
Vyama vyote vya siasa vinapaswa kuonesha bayana jinsi vinavyobeba ajenda ya watoto katika kampeni za uchaguzi kama njia mojawapo ya kuonesha utashi wa kisiasa katika kusaidia vijana kutokana na ukweli kwamba malezi bora kuanzia utotoni ndio yanayotoa kijana anayekuwa mpigakura bora.
Maandamano yalianzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa mpaka Uwanja wa Mashujaa ukijulikana zaidi kama Uhuru Platform leo jumanne tarehe 16, juni 2015. Wanafunzi wa Shule ya Adolph Kolping English Medium Primary School na Baadhi ya Watoto wa Shule nyingine za Manispaa ya Mukoba wameshiriki vyema siku ya hii ya leo Maalum ya Mtoto wa Afrika Ikibeba Ujumbe "Tokomeza Mimba na Ndoa za Utotoni" Picha na Faustine Ruta, Bukoba.
0 comments:
Post a Comment