Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel kupitia mpango maalumu wa Airtel Fursa, imeandaa warsha maalumu ya mafunzo ya ujasiriamali na namna ya kuendesha biashara zao kwa faida itakayofanyika mwanzoni mwa wiki ijayo.
Warsha hii itakayowajumuisha vijana kati ya miaka 18 - 24 wenye nia ya kujifunza na kujikwamua kiuchumi, inategemea kufanyika Jumatano ya tarehe 22/7/205, katika ukumbi wa Golden Rose hotel ulioko Arusha mjini kuanzia saa 2 asubuhi.
Akiongea na waandishi wa habari Meneja huduma za jamii wa Airtel Bi. Hawa Bayumi alisema, "Airtel Fursa imeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia na kuwawezesha vijana wengi nchini kupata elimu na pia kuwapatia misaada itakayowawezesha kuendesha biashara zao kwa ufanisi
"Mpaka sasa tumeshafanya semina kama hizi katika mikoa ya Dar es Saalam na Mwanza na kuwawezesha vijana zaidi ya 500 kupata mafunzo hayo muhimu ikiwemo usimamizi wa mtaji, mbinu za masoko, kuzitambia fursa na ujuzi wa kibiashara, namna ya kuendesha biashara na kuweka mahesabu , jinsi ya kufungua akaunti benki na nyingine nyingi"
Aliongeza kwa kusema "Kwa wakazi na vijana wa Arusha hii ni zamu yao sasa, tunatoa wito, wajitokeze kwa wengi kupata mafunzo haya bure bila gharama yoyote kupitia wataalamu wetu mahiri wenye ujuzi katika maswala ya biashara na ujasiriamali"
Tunaamini vijana wengi watatoka katika mafunzo haya wakiwa wamewezeshwa kuwa na mtazamo chanya lakini zaidi wakiwa na mbinu za kuendesha biashara zao kwa mafanikio zaidi.
Airtel kupitia Airtel Fursa itatoa warsha kama hizi maeneo mbalimbali ya nchi ambapo baada ya warsha hii kufanyika Arusha, wakazi na vijana wa mkoa wa Mbeya nao watafikia na kupata mafunzo katika wiki 2 zijazo.
0 comments:
Post a Comment