TFF, MSUVA, TAMBWE WAWASAIDIA VII

 Mchezaji Bora na Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, Simon Msuva wa Yanga, akiwakabidhi msaada wa chakula wanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Taifa, Temeke, jijini Dar es Salaam walioweka kambi shuleni kwao kujiandaa na mitihani ya Taifa itakayofanyika mwezi ujao.
NA MWANDISHI WETU

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), winga wa Yanga Simon Msuva na mshambuliaji wa klabu hiyo, Amissi Tambwe, wamewapiga tafu ya chakula wanafunzi wa darasa la saba wa Shule ya Msingi Taifa iliyopo Temeke, jijini Dar es Salaam walioweka kambi kujiandaa na mitihani ya taifa itakayoanza Septemba 9, mwaka huu.

Akizungumza na BINGWA jana, Mjumbe wa Kamati ya shule hiyo, Michael Maurus, alisema Msuva alitoa kilo 50 za mchele, ndoo ya mafuta ya kupikia na kiroba cha unga, wakati TFF ikitoa kilo 100 za mchele na Tambwe kilo 30 za mchele.

Alisema walifikia uamuzi huo wa kuomba msaada baada ya kudorora kwa michango ya wazazi, lakini pia uwepo wa watoto yatima na wasio na uwezo wa kuchangia kambi hiyo ya mwezi mmoja.

“Kwa niaba ya wazazi, walimu na wanafunzi, tunapenda kuwashukuru wote waliotusaidia ambao ni TFF, Msuva pamoja na Tambwe kwa kuonyesha kuguswa na jitihada zetu katika kuwaandaa ipasavyo vijana wetu wa darasa la saba kwa mitihani yao ya mwisho,” alisema Maurus na kuwataka wote walioahidi kuwasaidia kutosita kufanya hivyo.

Maurus alisema lengo la kuwaweka watoto hao kambini ni kuwawezesha kuelekeza akili zao zote katika masomo tayari kufanya maajabu kwenye mitihani ya Taifa mwezi ujao, wakiamini michezo mbalimbali ya majumbani imekuwa ikiwaathiri kwa kiasi kikubwa watoto kuzingatia masomo. Kwa upande wake, Msuva aliyefika shuleni hapo wiki iliyopita akiwa ameamabtana na baba yake, alisema:

“Nimewasaidia hawa wadogo zangu kwani binafsi huwa ninaguswa sana na suala la elimu, pia ifahamike wazazi wao ndio wanaoingia viwanjani kutusapoti tunapocheza, hivyo msaada huu ni sehemu ya shukrani zangu kwao.”
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment