Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (CCM) Bi. Zainabu Abdallah (katikati) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa pongezi kwa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kwa niaba ya Shirikisho hilo jana jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Habari (MAELEZO). Kushoto ni Katibu Msaidizi wa Shirikisho hilo Bw. Daniel Zenda na kulia ni Afisa Habari wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bw. Frank Mvungi.(Picha na Frank Shija).
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (CCM) Bi. Zainabu Abdallah akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) alipokuwa akitoa pongezi kwa Rais mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kwa niaba ya Shirikisho hilo jana jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Habari (MAELEZO).
Frank Mvungi, MAELEZO
Rais mteule wa Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa kwa kushinda kiti cha Rais katika uchaguzi mkuu ulifanyika oktoba 2015 ikiwa ni kielelezo cha utendaji bora alionyesha katika kuwatumikia watanzania kupitia nyazifa alizotumikia kabla ya kuchaguliwa katika nafasi hiyo.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa shirikisho la vyuo vikuu Chama cha Mapinduzi (CCM) Bi Zainab Abdallah wakati wa mkutano na waandishi wa Habari uliolenga kumpongeza Rais mteule kwa tiketi ya chama hicho.
“Akifafanua Bi Zainab amesema kuwa Rais Mteule Dkt. John Pombe Magufuli ameshinda kiti cha Urais kwa kuwa ndiye mtu pekee ambaye watanzania walikuwa wanamuhitaji ili aweze kuwaletea maendeleo kwa kuwa ni mchapa kazi na ameonyesha kwa vitendo dhamira hiyo katika utumishi wake kwa miaka yote iliyopita “alisisitiza Zainab.
Bi. Zainab amesema kuwa Rais mteule Dkt. Magufuli anayo dhamira ya dhati yakuwaletea maendeleo watanzania ndiyo sababu hata kauli mbiu yake ililisisitiza kuwa “hapa kazi tu” hivyo ni wajibu wetu kama watanzania kusisitiza umoja na mshikamano na kuondoa tofauti zetu ili tufanye kazi kwa bidii ili kujenga uchumi wa taifa.
Akizungumzia wasifu wa Rais Mteule Dkt. Magufuli; Bi Zainab amesema kuwa ni mtu mwenye uzalendo,mwadilifu,mchapa kazi, na ambaye watanzania wote wanamkubali kuwa anao uwezo wa kuliongoza Taifa katika kipindi hiki.
Kwa upande wa Uchaguzi mkuu Zainab amesema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki hali iliyowapa nafasi watanzania kuchagua viongozi wanaowataka na kupelekea chama cha mapinduzi kuongoza katika uchaguzi huo kutokana na utendaji madhubuti wa viongozi wa Chama na Serikali.
Pia Bi Zainab alitoa wito kwa watanzania kudumisha amani na umoja wa Kitaifa ulioasisiwa na Viongozi wa kwanza wa Taifa hili ili kufikia maendeleo ya Kweli.
Shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu Chama cha Mapinduzi (CCM) limekuwa likihamasisha vijana kufanya kazi kwa bidii ili kujenga Taifa.
0 comments:
Post a Comment