Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa CFIT kutoka UNESCO, Faith Shayo akizungumza machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda (hayupo pichani) kufungua rasmi mafunzo ya Tehama kwa walimu nchini.(Picha zote na Zainul Mzige wa Modewjiblog)
MAFUNZO kwa walimu watakaotumia teknolojia ya mawasiliano na habari (Tehama) kufundisha masomo ya sayansi ikiwamo hesabu yamefunguliwa katika maabara za Chuo Kikuu Huria jijini Dar es salaam.
Mafunzo hayo yanayohusisha walimu kutoka Vyuo vya Monduli, Tabora na Morogoro yamelenga kuoanisha ufundishaji na matumizi ya Tehama katika program ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya kuboresha elimu Tanzania kupitia ufadhili wa taifa la China.
Programu hiyo inayotoa ushirikiano mpya kati ya China na shirika hilo la Umoja wa Mataifa inafanyakazi katika mataifa manane ya kusini mwa jangwa la sahara inatekelezwa kwa lengo la kuwezesha mafanikio kwa malengo ya 2030.
Nchi zinaozhusika na mpango huo ni Tanzania Kongo ya Kinshasa (DRC), Congo, Liberia, Uganda, Côte d’Ivoire, Ethiopia na Namibia.
Mpango huo ambao kwa ujumla wake , awamu ya kwanza na ya pili unachukua miaka minne umelenga kuwezesha vyuo vya walimu kutoa walimu wa kufunza wenzao kwenye stadi za kufundisha kwa kutumia Tehama.
Mradi huo unaojulikana kama UNESCO-China Funds-in-Trust (CFIT) wenye lengo la kuziba pengo la ubora wa elimu wa kuwawezesha walimu kufundisha kwa kutumia Tehama ulizinduliwa Novemba 22,2012 kwa nchi tatu za kwanza na baadae kuongezwa nchi nyingine tano kufikia nane mwaka 2013.
Mpango huo ni wa dola za Marekani milioni 8 kutoka China mahususi kwa mataifa ya Afrika kuboresha elimu kupitia Unesco.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda akifungua mafunzo ya wiki mbili kwa walimu watakaotumia teknolojia ya mawasiliano na habari (Tehama) kufundisha masomo ya sayansi ikiwamo hesabu yanayoendelea katika maabara za Chuo Kikuu Huria (out) jijini Dar es salaam. Walioketi kutoka kushoto ni Basiliana Caroli Mrimi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa CFIT kutoka UNESCO, Faith Shayo pamoja na Kiongozi wa kitaifa wa timu ya mradi wa CFIT kit, Prof. Ralph Masenge.
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku 10 katika Chuo Kikuu Huria, Mtaalamu wa program za elimu kutoka makao makuu ya Shirika la Unesco mjini Paris, Ufaransa, Gabriel El Khili alisema kwamba program hiyo imelenga kutatua chnagamoto zinazokabili elimu ili elimu iwe ileinayotakiwa kuwezesha maendeleo ya kasi katika sayansi.
Alisema ni lengo la Unesco kupitia ufadhili huo kuhakikisha kwamba kunapatikana walimu bora watakaowezesha matumizi ya Tehama katika kufundisha masomo ya sayansi ikiwamo hesabu ili kutengeneza wataalamu wa baadae katika taifa hili.
Alisema kuna pengo kubwa kuhusiana na ubora wa elimu na kwamba baada ya kumaliza program ya elimu kwa wote mwaka jana nguvu sasa inastahili kuelekezwa katika ubora wa elimu ili kufikia malengo ya 2030.
Alisema changamoto kubwa ni kuleta karibu matumizi ya digitali kwa kuzingatia ukweli wa sasa kwamba matumizi yake ni madogo ukizingatia na haja kubwa inayoambatana na haja ya kuwa na elimu bora.
Alisema ni vyema kuiga mfano wa China kwamba kuna tatizo la kidunia la kielimu lakini linalohitaji suluhu ya eneo la husika kwa kuzingatia rasilimali zilizopo eneo hilo.
Mtaalamu wa program za elimu kutoka makao makuu ya Shirika la Unesco mjini Paris, Ufaransa, Gabriel El Khili (kulia) akizungumzia madhumuni ya programu hiyo inayoratibiwa na UNESCO wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ya wiki mbili kwa walimu yanayoendelea katika maabara ya Tehama Chuo Kikuu Huria (OUT) jijini Dar es Salaam.
Alisema mapinduzi ya kitamaduni ya China baada ya kujikomboa yalizingatia elimu na kwa kutumia rasilimali za nyumbani waliweza kusonga mbele na nia yao ya sasa ni kufikiri shida ya elimu na maendeleo kimataifa lakini kupata suluhu ya tatizo hilo kwa nchi husika kwa kuhakikisha rasilimali zilizopo zinatumika kuboresha elimu.
Anasema mafunzo kwa Tehama maana yake kusambaza elimu bora kwa kutumia nyenzo za Tehama zilizopo kuanzia redio televisheni, CD na kadhalika.
Alisema ni matumzi ya Unesco kwamba mafunzo yanayotolewa yatasaidia kuboresha elimu ya walimu na wanafunzi wao kwa kutumia Tehama, matumizi yake yaliyotukuka ambayo yatasaidia kuimarisha na kutoa ubora wa elimu pamoja na kuwa na walimu wachache.
Naye Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda akifungua mafunzo hayo aliwataka walimu hao kutambua umuhimu wao katika kusukuma mbele lengo la mafunzo hayo na wala si kujipatia cheti cha mahudhurio.
Kiongozi wa kitaifa wa timu ya mradi wa CFIT kit, Prof. Ralph Masenge akisisitiza jambo kwa washiriki wa mafunzo katika hafla fupi ya ufunguzi.
Alisema ulimwengu wa sasa ni wa walimu kutoa mwongozo wa namna ya kujifunza kwa kumuelekeza mwanafunzi kwa kuwa ulimwengu wa digitali umerahisisha mambo mengi.
Alisema wasishangae wakigundua kwamba wanafunzi wao ni weledi zaidi kuliko wao ila wasaidie kuhakikisha kwamba Tehama inatoa nafasi ya wanafunzi wengi kujifunza na kupata elimu wanayohitaji katika kubadili maisha na uchumi katika jamii.
Alisema kwamba ni matumaini yake kwamba kwa mafunzo hayo elimu ya Tanzania itapaa hasa kutokana na ukweli kuwa China imesema wazi kuwa haitapenda Tanzania kushindwa katika mradi huu wa kuleta maboresho makubwa katika elimu ya Tanzania ili iweze kutumika kutengeneza maarifa.
Profesa Bisanda alisema kwamba kwa sasa Tanzania ina shida kubwa katika masomo ya sayansi (bayolijia,kemia na fizikia ) pamoja na hesabu na kwamba uwapo wa program hiyo kutasaidia kufikisha mafunzo kwa wanafunzi kwa namna bora na yenye uhakika zaidi hata kama walimu wapo wachache.
Pichani juu na chini walimu kutoka Vyuo vya Monduli, Tabora na Morogoro wakishiriki mafunzo ya matumizi ya Tehama kwa vitendo katika program ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) ya kuboresha elimu Tanzania kupitia ufadhili wa taifa la China.
Alisema ni vyema walimu wakajifunza namna ya kufanya na kutafuta majawabu ya matatizo kwa kutumia tehama na kuambukiza mwenendo huo kwa wenzao na kwa wanafunzi.
Alisema ni kweli kuwa Tanzania ipo gizani katika ICT kutokana na matumizi yake madogo na hivyo walimu wakielewa na kuwafunza wengine taifa hili litaondoka katika giza hilo na kupata mapinduzi makubwa ya fikira na elimu.
Aidha alisema kwa kutumia ICT wanaweza kupunguza gharama za uendeshaji na uzalishaji hasa katika masomo na mafunzo.
Alitolea mfano kwamba kama wakipata softwea ya mitihani ambayo ipo wanaweza kuokoa zaidi ya shilingi milioni 700 wanazotumia kwa ajili ya mitihani na michakato yake.
“Fikiria unaweka program ambayo mwanafunzi anafanya mitihani moja kwa moja na hii inawezekana, utafanya nini na fedha hizo ambazo unazitumia sasa kwa ajili ya uandazi wa mitihani kuifanya na kuisahihisha” aliuliza na kusema kwamba zingelisaidia vitu vingine.
Alisema kihistoria walikuwa wanakazi kubwa ya kuandaa mitihani na kusambaza lakini mwanzo wa kuwafanya wanafunzi wajieleze kama wanataka kufanya mitihani kwa kutumia Tehama sasa wanatengeneza mitihani kwa kadiri ya maombi na kupunguza gharama.
Picha ya pamoja ya wakufunzi na washiriki.
Makamu wa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania (OUT), Prof. Elifas Bisanda (kushoto), Mtaalamu wa program za elimu kutoka makao makuu ya Shirika la Unesco mjini Paris, Ufaransa, Gabriel El Khili (katikati) pamoja na Mratibu wa kitaifa wa Mradi wa CFIT kutoka UNESCO, Faith Shayo (kulia) mara baada ya zoezi la picha ya pamoja.
0 comments:
Post a Comment