Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuwa makini na kuhakikisha vinazingatia ukweli, muda na maadili ya taaluma ya habari katika kuripoti taarifa kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2025, ili kulinda amani, mshikamano na usalama wa kitaifa.
Kauli hiyo imetolewa leo, Agosti 1, 2025, na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani Jacobs Mwambegelege, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa pamoja kati ya Tume na wahariri wa vyombo vya habari uliofanyika Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
“Vyombo vya habari ni daraja kati ya Tume na wananchi. Ni jukumu lenu kuhakikisha mnaleta taarifa zilizo sahihi, zisizopotosha na zenye lugha ya kujenga – siyo kubomoa. Hii ni kwa maslahi mapana ya mshikamano wa taifa letu,” amesema Jaji Mwambegele.
Ametangaza kuwa Tume imeandaa mafunzo maalum kwa wahariri na waandishi wa habari, yatakayofanyika Agosti 4, 2025, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa kuhusu sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Aidha, Mwenyekiti huyo amesema Tume imehusisha vyombo vya habari katika hatua mbalimbali za maandalizi ya uchaguzi ili kuongeza uwazi, uaminifu na ushirikishwaji wa wadau wote. Pia ameeleza kuwa taasisi na asasi 164 zimesajiliwa kutoa elimu ya mpiga kura, huku nyingine 88 zikitarajiwa kushiriki uangalizi wa uchaguzi.
Kwa upande wake, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) na Mhariri wa Clouds Media Group, Joyce Shebe, amesema wanahabari wana nafasi kubwa ya kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi kwa kutoa taarifa za uhakika.
“Elimu sahihi ni msingi wa demokrasia. Uwepo wetu hapa unaonyesha dhamira ya kweli ya kushirikiana na Tume kufanikisha uchaguzi huru na wa haki,” alisema Shebe.
Mhariri wa gazeti la Nipashe, Salome Kitomari, amesema mkutano huo umewapa wanahabari silaha muhimu kama sheria na miongozo ya uchaguzi ambayo itaongeza weledi wa kazi yao katika kipindi hiki nyeti.
Mwenyekiti wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Beda Msimbe alisisitiza wajibu wa wanahabari kuwa wazalendo kwa kuzingatia weledi na kutafuta chanzo sahihi cha taarifa kabla ya kuandika.
“Uandishi wa habari bila kujua chanzo sahihi unaweza kusababisha mkanganyiko na kuvuruga amani ya taifa letu. Tuwaelimishe Watanzania kwa usahihi, si kwa mihemko,” alionya Msimbe.
Naye Mhariri kutoka gazeti la Uhuru, Kiondo Mshana, ameshauri mafunzo kama hayo kuendelea kutolewa hata nje ya kalenda ya uchaguzi ili kuwajengea wanahabari uwezo wa kudumu katika taaluma yao, hususan kuhusu uandishi wa masuala ya uchaguzi.
Kwa ujumla, mkutano huo umebeba ujumbe mzito wa umuhimu wa ushirikiano kati ya vyombo vya habari na Tume, kwa lengo la kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa amani, haki na uwazi.
0 comments:
Post a Comment