
Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) kimewakutanisha viongozi wa matawi na waajiri zaidi ya 800 kutoka taasisi 300 za serikali kwa ajili ya mafunzo ya siku tano yanayolenga kuwajengea uwezo kuhusu matumizi ya Akili Mnemba (AI) na teknolojia za kidijitali katika kuimarisha afya na usalama sehemu za kazi.
Mafunzo hayo yameanza leo, Septemba 15, 2025 jijini Arusha na yatahitimishwa Septemba 19, yakijikita pia kwenye mada za taratibu za uendeshaji wa mashauri ya kinidhamu ya watumishi wa umma, usuluhishi na maamuzi ya kiutumishi, pamoja na mchango wa mabaraza ya wafanyakazi katika kukuza tija.
Katibu Mkuu wa TUGHE, Hery Mkunda, alisema mafunzo hayo yanagusa maeneo mengi muhimu ikiwemo mapambano dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia sehemu za kazi, afya ya akili na umuhimu wa emotional intelligence kwa viongozi na wafanyakazi.
Akifungua mafunzo hayo, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Zuhura Yunus, aliipongeza TUGHE kwa ubunifu huo akisema unaleta tija kwa serikali, wafanyakazi na taasisi.
“Ninaamini baada ya mafunzo haya, migogoro kazini itapungua na tija itaongezeka, kwani yanalenga kuunganisha waajiri na wawakilishi wa wafanyakazi katika kuelewa sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Joel Kaminyoge, alisema lengo ni kutoa elimu ya kiutumishi, kuimarisha mahusiano mema kazini, kuongeza tija na kuimarisha utawala bora sambamba na kupunguza migogoro.
Mshiriki wa mafunzo hayo, Neema Swai, alisema elimu hiyo ni muhimu kwa viongozi wa matawi kwani itawasaidia kupunguza migogoro sehemu za kazi. Aliipongeza serikali kwa kuridhia mfanyakazi anapojifungua mtoto njiti kupewa likizo maalumu kuanzia wiki ya 40 ya ujauzito.
Mafunzo hayo pia yanakwenda sambamba na safari ya kitalii ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa washiriki, ikiwa ni sehemu ya kujifunza na kutangaza vivutio vya utalii nchini.
0 comments:
Post a Comment