Mkuu wa Wilaya ya Chamwino: "Nchi Yetu Itajengwa kwa Kodi za Watanzania"

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja,akizungumza leo Septemba 26.09.2025 na timu ya maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha na kumtaarifu juu ya zoezi la kampeni ya elimu ya kodi mlango mlango wilayani humo.

Na Yahya Saleh-Chamwino

Chamwino, Dodoma – Ijumaa, 26 Septemba 2025: Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Mhe. Janeth Mayanja, amewataka wananchi wilayani humo kulipa kodi kwa wakati ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo ya Taifa.

Akizungumza na timu ya maafisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) walipofika ofisini kwake kwa ajili ya kujitambulisha na kutoa taarifa kuhusu kampeni ya elimu ya kodi kwa njia ya mlango kwa mlango, Mhe. Mayanja alisema:

"Hatuna nchi nyingine zaidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na nchi hii itajengwa na Watanzania wenyewe."

Ameeleza kuwa miradi yote ya maendeleo nchini, ikiwemo barabara, shule, na huduma za afya, inatekelezwa kupitia kodi zinazolipwa na wananchi. Hivyo, amewataka wote wenye sifa za kulipa kodi kuhakikisha wanatimiza wajibu huo bila kusubiri kushinikizwa.

Aidha, Mhe. Mayanja aliipongeza TRA kwa kufanikisha ukusanyaji wa mapato kwa ufanisi na kuvuka malengo ya makusanyo, huku akiisisitiza kuongeza jitihada zaidi ili kufanikisha maendeleo ya Taifa.

"Naomba muendelee kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato na mjitahidi kuwafikia walipakodi walioko kwenye kata na vijiji mbalimbali ili sote kwa pamoja tuchangie maendeleo ya nchi yetu," aliongeza.

Kwa upande wake, Meneja wa TRA Wilaya ya Chamwino, Bi. Ester Mallya, alisema mamlaka hiyo imejipanga kuongeza ushirikiano na Watendaji wa Kata pamoja na Wenyeviti wa Mitaa ili kuhakikisha elimu ya kodi inawafikia wananchi wote.

Bi. Mallya alibainisha kuwa sambamba na elimu hiyo, TRA pia itahakikisha inawasajili wananchi wote wenye wajibu wa kisheria wa kulipa kodi.

Kampeni ya elimu ya kodi mlango kwa mlango wilayani Chamwino inalenga kuongeza uelewa wa wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi na mchango wao katika kujenga Taifa lenye uchumi imara.

SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment