




Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT) limetangaza kikosi cha timu ya taifa ya mabondia 26 pamoja na benchi la ufundi lenye watu 9, kitakachoiwakilisha nchi katika Mashindano ya Kanda ya 3 Afrika yatakayofanyika Nairobi, Kenya kuanzia Oktoba 14 hadi 25, 2025.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, imeeleza kuwa kikosi hicho kimeteuliwa kufuatia mashindano ya Klabu Bingwa ya Taifa yaliyomalizika hivi karibuni, na sasa kiko tayari kupambana ili kuipatia Tanzania heshima katika jukwaa la kimataifa.
Mashindano ya Nairobi yanatarajiwa kuwa jaribio la kwanza la kimataifa kuelekea maandalizi ya michezo ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth Games) yatakayofanyika Glasgow, Scotland kuanzia Julai 23 hadi Agosti 2, 2026, ambapo Tanzania itashiriki rasmi.
Kwenye orodha ya mabondia walioteuliwa, upande wa wanaume unaongozwa na Juma Athumani (MMJKT) atakayepigania uzito wa 46-48kg (minimumweight), Azizi Chala (Ngome) uzito wa 48-51kg, na Faki Issa wa Jeba Tanga (bantamweight). Pia wamo bondia machachari kama George Costantino (Ngome), Ezra Paulo (Ngome), Rashid Mrema (Polisi), pamoja na Maximillian Patrick (MMJKT) atakayepigania uzito wa juu kabisa, super heavyweight (92kg+).
Kwa upande wa wanawake, timu inajivunia vipaji vya mabondia kama Martha Kimaro (Ngome), Aisha Hamisi (JKT), Sarafina Fusi (Ngome), pamoja na Veronica Ebroni (Magereza) ambaye atawakilisha taifa kwenye uzito wa juu (heavyweight).
Aidha, benchi la ufundi linaongozwa na Samwel Kapungu (Mwalimu Mkuu - BFT) akisaidiana na Mzonge Hassani (Ngome), pamoja na walimu wengine kutoka MMJKT, Ngome na Polisi. Pia kuna waamuzi, matron Fatuma Manzi (MMJKT) na daktari wa timu Mussa Magolima (BFT).
Akizungumzia maandalizi hayo, Mashaga alisema kuwa Tanzania ina matarajio makubwa kutokana na maandalizi mazuri na ari ya wachezaji waliochaguliwa.
“Tunakwenda Nairobi tukiwa na dhamira ya dhati ya kupima kiwango chetu na kuhakikisha tunaandaa timu imara kuelekea michezo ya Jumuiya ya Madola 2026. Kikosi hiki kina wachezaji wenye vipaji na uzoefu wa kutosha,” alisema.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa kivutio kikubwa, huku Tanzania ikitarajia kufanya vizuri na kushinda medali ili kuendelea kujijengea heshima katika ramani ya ngumi za kimataifa.
Mgombea Ubunge wa Viti Maalum Mkoa wa Pwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mariam Ibrahim, amewataka wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi na kumpigia kura Mgombea Urais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na wagombea wengine wa chama hicho.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni uliofanyika wilayani humo jana Septemba 17, 2025, Mariam alipiga magoti mbele ya wananchi akisisitiza mshikamano na mshikikano wa kisiasa kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Mariam alisema ni muhimu Rais Samia, Mgombea Ubunge wa Bagamoyo Subira Mgalu, na madiwani wa CCM katika kata mbalimbali wakapewa kura nyingi ili kuendeleza miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali.
Aidha, aliwahimiza wanawake kushirikiana kikamilifu katika kampeni na kuhamasisha jamii nzima kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi, akibainisha kuwa ushiriki wao ni nyenzo muhimu ya kuendeleza maendeleo ya Bagamoyo na taifa kwa ujumla.