BILIONI 8 KUTUMIKA KUBORESHA VYUO VYA AFYA NCHINI

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Hamis Kigwangala.

Na. Aron Msigwa - Dodoma.

Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilioni 8 kuboresha miundombinu ya vyuo vya Afya kote nchini katika mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuwawezesha wanafunzi wa fani ya Afya kusoma katika mazingira mazuri.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Hamis Kigwangala ameyasema hayo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Muhambwe Mhe.Atashasta Justus Ntitiye, alieyata kujua mkakati wa Serikali wa kuboresha vyuo vya Afya nchini hususan chuo cha Uuguzi wilayani Kibondo kilicho katika jimboni lake. 

Dkt.Kigwangala amesema Serikali katika mwaka wa fedha 2016/2017 imejipanga kuboresha mazingira ya vyuo vya Afya katika maeneo mbalimbali nchini kikiwemo Chuo cha Uuguzi Kibondo ambacho kimetengewa shilingi milioni 680.

Aidha, ameeleza kuwa vyuo vya Afya vimekuwa vikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo madeni ya wazabuni wa vyakula waliokuwa wakiidai Serikali kiasi cha shilingi Bilioni 6.8 kuanzia mwaka 2009 hadi 2015.

Amebainisha kuwa tayari Serikali imekwishahakiki madeni yote ya wazabuni ili yaweze kulipwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 na kuongeza kuwa suala la usambazaji wa vyakula limeachwa chini Sekta binafsi ili zifanye kazi hiyo.

Katika hatua nyingine Dkt.Kigwangala amesema Serikali inaendelea kuangalia uwezekano wa kuyatumia majengo yaliyoachwa kwenye kambi za wakimbizi zilizofungwa mkoani Kigoma hususan wilayani Kibondo ili yaweze kutumika kama vyuo vya kutolea elimu ya Afya.

" Niko tayari nikishirikiana na waheshimiwa wabunge kwenda mkoani Kigoma kuzungumza na viongozi wa mkoa huo ili tuweke utaratibu wa namna ya kuyatumia majengo hayo" Amesisitiza Dkt.Kigwangala.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment