Daktari wa macho akiwa katika jukumu la kumpima macho mwanafunzi wa shule ya msingi Msasani jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya madaktari wakiwa katika majukumu yao ya kuhakikisha kila mwanafunzi anapata matibabu.
Rais wa klabu ya Rotary ya Oyster bay jijini Dar es Salaam, Bwana Mohammed Versi akizungumza na wanahabari.
---
Klabu
ya Rotary ya Oyster Bay ya jijini Dar es Salaam imeandaa kambi ya matibabu na
kutoa huduma za afya kwa wanafunzi wa shule mbili za Msasani, Msasani A na
Msasani B na kufanikiwa kutoa huduma kwa wanafunzi zaidi ya 950. Kambi hiyo ya
siku moja ilitoa vipimo vya afya, ushauri, matibabu na huduma mbalimbali za
meno, macho, malaria, usafi wa mwili, minyoo, masikio, pua na koo (ENT), pamoja
na magonjwa ya ngozi. Kampeni ya Damu Salama pia ilifanyika wakati wa kambi
hiyo ili kuwawezesha uchangiaji wa damu katika benki ya damu salama.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Rais wa klabu ya Rotary ya Oyster bay jijini Dar es
Salaam, Bwana Mohamed Versi alisema waliguswa kufadhili upimaji huo kwa sababu
suala la afya ni jambo la msingi kwa mwanadamu
"Rotary
tumekuwa na utaratibu wa kusaidia jamii, na hii si mara ya kwanza kusaidia
shule hii, tayari tumeshajenga maktaba mbili, tumeweka maji safi na salama,
tumepanda miti, tumejenga ukuta ili kuimarisha ulinzi na awamu hii tumeona ni vyema tutoe huduma ya
afya"
Uongozi
wa shule ya msingi Msasani umesema umefurahishwa na kitendo cha klabu ya Rotary
ya Oyster Bay kwa kutambua kuwa afya njema ni silaha bora kwa mtoto katika
mafaniko ya kielimu.
"Nawashukuru
mno Rotary maana wamekuwa washirika waaminifu wa vitendo na si maneno pekee.
Bado tunaomba wadau wengine waige mfano huu katika kutusaidia, bado tuna
changamoto mbalimbali zinazotukabili" alisema mwalimu mkuu wa shule hiyo,
Egidius Mjumangoma
Kambi
hiyo ya matibabu ni muendelezo wa huduma mbalimbali za kijamii zinazotolewa na
klabu hiyo katika shule za Msasani A na B. Miradi katika shule hiyo ilianza
katika eneo la maji na usafi ambapo shule hizo zilipatiwa maji safi na salama
ya kunywa pamoja na ya matumizi mengine. Klabu hiyo pia ilifanya ukarabati wa
majengo na kuweka vitabu katika maktaba mbili kwenye shule hizo. Maktaba hizo
zina vitabu vipya na vinavyovutia kwa matumizi ya watoto, makabati yenye vitabu
vipya vipatavyo elfu nne (4,000) vingi vikiwa katika lugha ya Kiswahili, ili
kutoa hamasa ya kusoma kwa watoto wadogo.
Klabu
hiyo ya Rotary Oyster Bay, kwa sasa iko katika ujenzi wa ukuta kuzunguka shule
hizo ili kuweka usalama wa mali za shule pamoja na wanafunzi. Ujenzi huo
umewezeshwa na fedha zilizopatikana kutoka kwenye mojawapo ya shughuli za
ukusanyaji fedha zinazofanywa na klabu hiyo. Mojawapo ya kazi zilizofanyika
wakati wa kambi ya matibabu ilikuwa ni ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa
ukuta huo ambapo wanaklabu na wageni waalikwa walishiriki katika ziara hiyo.
Kambi
hiyo ya matibabu imefanyika kwa udhamini wa Diamond Trust Bank, Whitedent,
Knight Support, Vital Supplies, Mansoor Daya, Cello na Sayona kwa ushirikiano
na Hindu Mandal Hospital, TDA, Damu Salama na wanafunzi kutoka Muhimbili
University of Health and Allied Sciences (MUHAS) na Hubert Kairuki Memorial
University (HKMU).
Maktaba
hizi mbili zilifadhiliwa chini ya mpango uitwao “Rotary Global Grant”, ambapo
katika tafsiri za Rotary, ni pale ambapo Rotary International na ofisi ya
Rotary katika kanda husika hutoa msaada wa kifedha kwa klabu yoyote ya Rotary
ndani ya kanda. Klabu inayopewa ufadhili huo inatakiwa kushirikiana na klabu
yoyote kutoka kanda nyingine ili kuendesha mradi wa jamii ulio endelevu na
ambao matokeo yake yanaweza kupimika.
Baada
ya shule hizo kuchukuliwa chini ya uangalizi wa Klabu ya Rotary ya Oyster Bay,
miradi mingine inapangwa kufanyika katika shule hizo mbili ambapo mafunzo kwa
walimu yameandaliwa kufanyika ndani ya mwaka huu. Walimu wa shule hizo watapewa
mafunzo ya namna ya kufundisha watoto, yani namna na kutumia maktaba hizo mpya
kwa lengo la kukuza kiwango cha uelewa kwa watoto wadogo kwenye jamii zetu.
0 comments:
Post a Comment