Kutokana na machafuko yanayoendelea nchini Burundi na kusababisha kufurika kwa waomba hifadhi nchini hususani mkoa wa Kigoma, kambi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu imejaa na kusababisha shule zilizopo ndani ya kambi hiyo kufungwa kwa muda.
Akizungumza na katika kambi hiyo, mkuu wa kambi hiyo, Sospeter Boyo, alisema uwezo wa kambi hiyo kwa sheria za kitaifa ni kuhifadhi wakimbizi 50,000 lakini kwa sasa ina watu 54,706 ambao ni wazamani.
“Kwa kawaida kambi hii ina uwezo wa watu 50,000 kulingana na taratibu za kimataifa, lakini mpaka sasa ina wakimbizi 54,706... hivyo baada ya kuanza kuwapokea waomba hifadhi wapya Aprili 29, mwaka huu, tumepata wapya 16,808 hadi juzi,” alisema Boyo.
Alisema, hata hivyo licha ya kufunga shule zilizopo kambini hapo, lakini wataendelea kuwapokea wageni hao kutokana na serikali ya mkoa kutafuta eneo lingine litakalokuwa na uwezo wa kuchukua wakimbizi wengi zaidi.
Alisema kwa sasa wamefunga shule ili majengo hayo yaweze kutumika kuwahifadhi wahamiaji wapya wanaowasili kila siku kutoka kitongoji cha Kagunga wilayani Kigoma, wanaokochukuliwa na meli ya Mv Liemba.
Hata hivyo, alisema huduma zote muhimu zinapatikana vizuri kambini hapo kuanzia chakula, maji, afya pamoja na watoa huduma wa mashirika mengine kuwapo kambini hapo.
Aidha, alisema kambi hiyo inakusudiwa kuwasiliana na viongozi wa dini wa makanisa na misikiti ndani ya kambi hiyo ili kuweza kusitisha huduma zao kwa muda, kwa lengo la kuwaweka waomba hifadhi hao ambao kwa sasa wamekuwa wengi.
Baadhi ya wakimbizi kambini hapo, walisema kitendo cha kushindwa kuondolewa madarakani kwa Rais Pierre Nkurunzinza, kimewasikitisha kwani kitasababisha kuwapo na machafuko zaidi.
Wakizungumza huku wakiomba kutotajwa majina yao kwa hofu ya kuvamiwa na wafuasi wa Nkurunzinza, walisema kuondoka Burundi hawakupenda, lakini imewalazimu kutokana na uonevu unaofanywa na kikosi maalum cha Rais huyo kiitwacho ‘mbonerakulaa’ kinachodaiwa kufanya mauaji kwa watu wenye itikadi tofauti na Nkurunzinza.
“Tunasikitika sana kwa jaribio hilo kutofanikiwa, sasa hali itakuwa mbaya zaidi nchini kwetu kutokana na machafuko ya kushindwa kuondolewa madarakani Nkurunzinza,” alisema mmoja wa wakimbizi hao.
Mkimbizi mwingine katika kambi hiyo alisema awali walikuwa na furaha waliposikia Nkurunzinza ameondolewa madarakani kwani kungesaidia kupatikana kwa amani.
Alisema kuhangaika kila mara kwa wananchi wa Burundi kuomba hifadhi nchi jirani, kunatokana na demokrasia Burundi kupotea pia kufanyika kwa mauaji ya kimya kimya kwa wananchi wake hususani wale wenye mlengo tofauti na Rais aliyopo madarakani.
Afisa Uhamiaji mfawidhi wa Kagunga, Boniface Mayala, alisema mpaka jana waliongozeka wakimbizi 108 na kufikisha idadi ya walioingia mpaka sasa kufikia 90,000. “Zaidi ya 11,000 tayari wamesafirishwa kwenda mjini tayari kupelekwa kambini kwa ajili ya uhifadhi,” alisema Mayala.
0 comments:
Post a Comment