KAPUYA APINGA KISWAHILI KUTUMIKA KUFUNDISHIA

SERIKALI imehadharishwa kutowatenga Watanzania na ulimwengu kwa kutekeleza sehemu ya Sera ya Elimu, inayotaka Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia kutoka shule ya awali mpaka chuo kikuu. 

Mbunge wa Urambo Magharibi, Profesa Juma Kapuya, ametoa hadhari hiyo bungeni jana wakati alipokuwa akichangia katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu unaoendelea. Profesa Kapuya alikumbusha maoni ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliposema kuwa Ki ingereza ndio Kiswahili cha dunia. 

Profesa Kapuya amewahi kuwa waziri wa elimu na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Alionya kuwa Watanzania watafanya kosa kubwa litakalowagharimu katika Jumuiya za kikanda hasa katika ushindani wa ajira, kama wataondoa Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia. 

Alitoa mfano wa nchi ya Rwanda, ambayo imebadilisha lugha ya kufundishia kutoka Kifaransa kwenda Kiingereza na kuongeza; “Nenda pale Rwanda uone mtoto wa darasa la saba anavyozungumza Kiingereza kizuri.” 

Aliwajia juu wanaoshabikia Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia kutoka shule ya awali mpaka chuo kikuu, kwamba ni wanafiki kwa kuwa wenyewe watoto wao wamewapeleka katika shule za mchepuo wa Kiingereza. 

Alisema watua hao wamekuwa wakitoa mfano wa China na Japan, lakini wanasahau kuwa nchi hizo zina historia tofauti ya elimu ikilinganishwa na nchi za Afrika hususani Tanzania. 

“Kule Afrika Kusini wakati wa mauaji ya Soweto, moja ya madai ya Waafrika Kusini ni kuacha kufundishwa kwa kutumia lugha ya Afrikaans na Kizulu, na badala yake wafundishwe kwa Kiingereza ili wawe sehemu ya ulimwengu,” alisema Profesa Kapuya. 

Alionya kuwa kama Serikali itaendelea na mpango huo wa kutekeleza sehemu ya Sera ya Elimu ili Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia, hatari ya kwanza itakuwa kulazimisha baadhi ya watu kujifungia na kuanza kutafsiri mawazo ya watu. 

Alifafanua kuwa kwa mazingira hayo, itakuwa sawa na kulazimisha watu kutunga vitabu, wakati kiuhalisia watu hujiamulia kuandika vitabu wenyewe. Hatari ya pili kwa mujibu wa Profesa Kapuya, ni kuwanyima Watanzania hasa waliomaliza vyuo vikuu, wigo wa kujisomea vitabu mbalimbali na kupata maono na kujiwekea dira zao binafsi. 

Profesa Kapuya aliwahi kuwa Waziri wa Elimu, Utamaduni na Michezo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana. Alihitimu Shahada yake ya Sayansi katika Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1971 na pia Shahada ya Pili ya Sayansi katika Botani katika chuo kikuu hicho mwaka 1972.

Alipata Shahada ya Udaktari wa Falsafa katika Botani katika Chuo Kikuu cha Wales Aberystwyth. Baada ya kuhitimu UDSM, Profesa Kapuya aliajiriwa moja kwa moja kufundisha katika chuo kikuu hicho, akianzia Mhadhiri Msaidizi wa Botani, Mhadhiri, Mhadhiri Mwandamizi hadi Profesa wa Botani. 

Aligombea ubunge wa Urambo Magharibi mwaka 1995 na kushinda. Alishinda tena ubunge katika uchaguzi wa 2000, 2005 na 2010.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment