NACTE YAPATA MAFANIKIO MAKUBWA KATIKA KIPINDI CHA MIAKA 10

Mkurugenzi wa Idara ya Ushauri na malezi wa vyuo(NACTE).Dkt. Adolf Rutayuga(katikati) akiongea na waandishi wa habari(hawapo pichani)kuhusiana na manifanikio ya usajili wa taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi yaliyopatikana katika kipindi cha serikali ya awamu ya Nne ambapo umeongezeka kutoka 168 mwaka 2005 hadi 528 mwaka 2015 huku 206 vikiwa ni vya Serikali na 322 si vya Serikali.Wanaoshuhudia kushoto ni Mkurugenzi wa Ukuzaji na Urekebishaji Mitaala Bi. Twilumba Mponzi na Mkurugenzi wa Udhibiti,Ufuatiliaji na Tathimini Bi. Agness Ponera.
Baadhi ya waandishi wa habari wakiwa wanamsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Ushauri na malezi wa vyuo(NACTE).Dkt. Adolf Rutayuga(katikati) wakati alipokuwa akiongea nao kuhusiana na manifanikio ya usajili wa taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi yaliyopatikana katika kipindi cha serikali ya awamu ya Nne ambapo umeongezeka kutoka 168 mwaka 2005 hadi 528 mwaka 2015 huku 206 vikiwa ni vya Serikali na 322 si vya Serikali.Wanaoshuhudia kushoto ni Mkurugenzi wa Ukuzaji na Urekebishaji Mitaala Bi. Twilumba Mponzi na Mkurugenzi wa Udhibiti,Ufuatiliaji na Tathimini Bi. Agness Ponera.
---
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) limeelezea mafanikio makubwa liliyoyapata katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne (2005-2015) huku likitoa wito kwa wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi kutoa mchango wao wa hali na mali ili kuboresha elimu na mafunzo hayo nchini.

 Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dkt. Adolf Rutayuga ambaye ni Mkurugenzi wa Ushauri na Malezi kwa vyuo vya Ufundi, alisema usajili wa taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi umeongezeka kutoka 168 mwaka 2005 hadi 528 mwaka 2015 huku 206 vikiwa ni vya Serikali na 322 si vya Serikali.

 Dkt. Rutayuga alieleza kuwa, kwa mujibu wa Sheria iliyoanzisha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Na. 9 ya mwaka 1997) vyuo na taasisi za serikali na binafsi zinazotoa elimu na mafunzo ya ufundi zinatakiwa kusajiliwa na kupata ithibati ili ziweze kuendesha mafunzo. 
 Akizungumzia suala la ithibati ya taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi alisema pamoja na usajili, taasisi (chuo) ya elimu na mafunzo ya ufundi inatakiwa iwe na ithibati ili kuweza kufikia kiwango cha ubora unaostahili wa mafunzo yatolewayo na kuongeza kuwa kwenye kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi vyenye Ithibati vimeongezeka kutoka 59 mwaka 2005 hadi 122 mwaka 2015 ambapo 84 ni vya serikali na 38 si vya serikali. 
 Kuhusiana na mitaala inayozingatia umahiri na mahitaji ya soko la ajira alieleza kuwa, mojawapo ya masharti ya usajili na ithibati kwa taasisi (chuo) ya elimu na mafunzo ya ufundi ni kuwa na mitaala iliyoidhinishwa na Baraza na kufafanua kuwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne Baraza limefanikisha ongezeko la mitaala inayozingatia umahiri na mahitaji ya soko la ajira (compence-based and demand-driven curricula) iliyoidhinishwa kutumika katika taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi kutoka 17 mwaka 2005 hadi 412 mwaka 2015. 
 “Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne, Baraza limefanikiwa kuanzisha Mfumo wa kielektroniki wa udahili wa pamoja (Central Admission System) wa wanafunzi katika taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi nchini. 
"Kwa kushirikiana na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) katika mwaka wa masomo 2012/2013 jumla ya wanafunzi 2, 552 walidahiliwa. Katika mwaka wa masomo 2013/2014 idadi hii ilizidi kuongezeka ambapo jumla ya wanafunzi 9,320 walidahiliwa kujiunga na taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi vinavyotoa Shahada. 
"Vilevile, pamoja na Shahada mfumo huu umeliwezesha Baraza kuongeza programu zaidi kama vile Stashahada za Afya na Stashahada za Ualimu. Ongezeko hili la programu limeliwezesha Baraza kudahili wanafunzi wengi zaidi ambapo kwa mwaka wa masomo 2014/2015 wanafunzi 63,498 walidahiliwa,” alieleza. 
 Aliongeza kuwa, mfumo huo wa Kieletroniki wa Udahili wa Wanafunzi, pamoja na mfumo wa zamani ambao si wa kieletroniki imewesha kuongezeka kwa wanafunzi waliodahiliwa katika taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi kutoka 40,059 mwaka 2005 hadi 113,080 mwaka 2015. 

Mkururugenzi huyo alisema sheria iliyoanzisha Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, inalitaka Baraza kuhakiki na kusajili walimu wenye sifa za kufundisha katika taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi nchini. 

“Katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Nne Baraza limefanikisha ongezeko la walimu waliosajiliwa ambao wanafundisha katika taasisi na vyuo vya elimu na mafunzo ya ufundi kutoka 271 mwaka 2005 hadi 3,067 mwaka 2015,” alieleza. 
 Dkt. Rutayuga alisema katika kipindi hicho pia ili kufikisha huduma karibu na wadau wa elimu na mafunzo ya ufundi nchini, Baraza limeanzisha ofisi nane za kanda zilizopo katika mikoa ya Mwanza, Dodoma, Dar es Salaam, Mtwara, Mbeya, Katavi, Zanzibar na Arusha.
SHARE
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment